Mapambano dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya!
Padre Federico Lombardi anasema kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anaunga mkono mapambano
dhidi ya biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya yanayofanywa na watu mbali
mbali na kwamba, matumizi ya maneno "evitar la mexicanizacion" katika
ujumbe aliomwandikia rafiki yake kutoka Argentina hauna uhusiano wowote na wananchi
wa Mexico, bali ni msemo uliokuwa umetumiwa kwenye e mail yake binafsi kutoka kwa
rafiki yake. Ufafanuzi huu umetolewa kwenye Ubalozi wa Mexico mjini Vatican.
Baba
Mtakatifu anawapenda, anawaheshimu na kuwathamini wananchi wa Mexico na kwamba, anapenda
kuwaalika wananchi na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kupinga biashara
na matumizi haramu ya dawa za kulevya kwani yana madhara makubwa kwa jamii. Mexico
na Amerika ya Kusini katika ujumla wake ni eneo ambalo limeathirika sana kwa biashara
na matumizi haramu ya dawa za kulevya.
Kumbe, mapambano dhidi ya biashara
hii hayana budi kupewa kipaumbele cha pekee na Serikali pamoja na wadau mbali mbali,
ili kupambana na vita pamoja na ukosefu wa amani, jambo linachochewa kwa kiasi kikubwa
na biashara haramu ya dawa za kulevya.
Baba Mtakatifu Francisko kwa nyakati
na mara kwa mara alipokutana na kuzungumza na Maaskofu amekazia umuhimu wa Jumuiya
ya Kimataifa kuwa na mikakati na sera makini za kupambana na biashara na matumizi
haramu ya dawa za kulevya kwa kushirikiana kwa vitendo.
Na Padre Richard A.
Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican