2015-02-24 09:49:02

Msiwageuzie maskini kisogo!


Katika maadhimisho ya Mwaka wa Maskini nchini Ufilippini waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaalikwa kujenga mshikamano wa upendo na udugu, ili kuong'a tofauti za matabaka ambazo zimekuwa ni chanzo za kinzani za kijamii na ukosefu wa amani na maridhiano nchini humo. Jamii isiwaguezie maskini kisogo, bali ihakikishe kwamba, maskini wanasaidiwa kupata mahitaji yao msingi katika maisha.

Ni changamoto inayotolewa na Kardinali Louis Tagle, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Manila, Ufilippini wakati huu wa maadhimisho ya Kipindi cha Kwaresima. Hapa kuna haja kwa Familia ya Mungu nchini Ufilippini kujifunga kibwebwe ili kupambana na ubinafsi pamoja na uchoyo mambo ambayo yanawafanya watu kugubikwa na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani zao.

Watu wajitahidi kupambana kufa na kupona na ukosefu wa haki msingi za kijamii, rushwa na ufisadi; baa la njaa na utapiamlo wa kutisha miongoni mwa watoto wenye umri chini ya miaka sita, ambao wengi wao wanafariki dunia kwa kukosa chakula bora. Haya ni mambo ambayo yako ndani ya jamii, kumbe, kipindi cha Kwaresima kiwasaidie watu kufanya toba na wongofu wa ndani, tayari kuwaonjesha jirani zao upendo na huruma ya Mungu.

Hiki ni kipindi kinachowahamasisha waamini kuyapyaisha maisha yao ya kiroho kwa njia ya sala na tafakari ya Neno la Mungu inayomilishwa katika matendo ya huruma. Hapa waamini washiriki kikamilifu katika sera na mikakati ya Jimbo katika mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo. Sala wakati wa Kwaresima inakwenda sanjari na umwilishaji wa mshikamano wa upendo na udugu, ili kukuza na kudumisha amani na maridhiano kati ya watu.

Wananchi wanahamasishwa kuwasaidia na kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii sanjari na utunzaji bora wa mazingira kwani athari za mabadiliko ya tabianchi bado zinaendelea kuwatumbukiza wananchi wengi katika lindi la umaskini wa hali na kipato pamoja na magonjwa ya mlipuko. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wajitahidi kutomezwa na utamaduni wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.