Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Bibi Amina
Masenza aandae orodha ya watumishi wa mkoa huo ambao wamekaa kwenye nafasi za ajira
kwa zaidi ya miaka 10 na kumpelekea ili wafanyiwe utaraibu wa kuhamishiwa vituo vingine. Ametoa
agizo hilo Jumatatu, Februari 23, 2015 wakati akizungumza na viongozi mbalimbali wa
mkoa wa Iringa waliofika kusikiliza majumuisho ya ziara ya siku sita ya Waziri Mkuu
kwenye mkoa huo. Mkutano huo ulifanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Mufindi ulioko Mafinga, wilayani Mufindi. “Tafuta wote waliokaa zaidi ya miaka 10.
Ni lazima tuwabadilishe... niletee orodha mapema iwezekanavyo,” alisema Waziri Mkuu. Alisema
nia ya zoezi hilo ni kuongeza ufanisi kwani watumishi wakikaa sehemu moja kwa muda
mrefu wanakuwa butu kwa kukosa ubunifu kwenye kazi zao, wanaota mizizi na kugeuka
kuwa chanzo cha matatizo katika baadhi ya sehemu. Alimtaka pia Mkuu huyo wa mkoa pamoja
na timu yake wasimamie vizuri ukusanyaji wa mapato ili kuongeza kiwango cha mapato
cha mkoa huo. “Na siyo hilo tu, simamieni vizuri matumizi ya fedha zilizopangwa kwenye
miradi mbalimbali ili kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi mnaowaongoza,” alisisitiza. Alisema
mkoa wa Iringa ni wa pili kwa kuwa na kiwango cha juu cha pato la mwanachi wa kawaida
baada ya Dar es Salaam ambao ndiyo unaongoza nchini. “Katika taarifa ya Mkuu wa Mkoa,
tulielezwa kwamba pato la mwananchi wa Iringa katika mwaka 2013 lilikuwa ni wastani
wa shilingi 1,660,532/- ambazo ni sawa na shilingi 138,377/- kwa mwezi au shilingi
4,612/- kwa siku”. Alisema pato la mwananchi wa Iringa linakua vizuri ikilinganishwa
na mwaka 2006 ambapo pato hilo lilikuwa shilingi 589,607/- na limeongezeka hadi kufikia
shilingi 1,660,532/- mwaka 2013. Alivitaja viashiria vya kukua kwa uchumi kuwa ni
pamoja na ujenzi wa nyumba za kisasa zenye umeme, elimu bora, afya bora na upatikanaji
wa vifaa vya mawasiliano kwenye ngazi ya kaya. Alisema kulingana na taarifa ya
Shirika la Fedha Duniani (IMF), Tanzania imeondolewa kutoka miongoni mwa nchi 10 barani
Afrika zenye umaskini mkubwa na kwamba sasa Tanzania ni miongoni mwa nchi 20 duniani
ambazo uchumi wake unakua kwa kasi kubwa. “Kukua kwa pato la mkoa kumechangiwa
hasa na kuwepo kwa mashamba makubwa ya tumbaku, chai, viwanda vya chai, misitu na
viwanda vya mbao. Tukitumia vizuri fursa hizi, na tukijipanga vizuri tutaweza kuongeza
pato la mkoa kuzidi hapa tulipo,” alisema. Aliwataka watendaji wote katika ngazi
zote, wawe na dhamira ya kuwaletea wananchi maendeleo na hivyo kuwaondolea umaskini
na kuongeza pato lao kwa kila mmoja. “Ninawasihi sana viongozi wa mkoa tutangulize
maslahi ya wananchi na siyo maslahi yetu binafsi. Tukifanya hivyo, wananchi wataona
kweli tunawasaidia na tunastahili kuwaongoza,” aliongeza.
Waziri Mkuu amemaliza
ziara ya siku sita katika mkoa wa Iringa na leo anakwenda Makambako, Njombe kuzindua
uandikishaji wa Daftari la Mpiga Kura. Baadaye mchana, ataelekea Mbeya kuanza ziara
ya kikazi ya siku sita kukagua shughuli za maendeleo katika mkoa huo.