2015-02-24 09:56:57

Jiografia ya maisha ya Nabii Eliya!


Wahudumu na Manabii wa Mungu aliye hai ndiyo mada inayoongoza mafungo ya maisha ya kiroho yanayotolewa na Padre Bruno Secondin kwa Baba Mtakatifu Francisko pamoja na wasaidizi wake wa karibu huko Ariccia, nje kidogo ya mji wa Vatican. Jumapili jioni, tarehe 22 Februari 2015 walianza mafungo kwa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, katika hali ya ukimya.

Wanamafungo walialikwa kutoka katika undani wao, tayari kuanza safari, itakayowasaidia kujifunza huruma ya Mungu kama ilivyokuwa kwa Nabii Eliya, ili kuwaendea maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, tayari kuwaonjesha Injili ya Furaha. Padre Secondin anawaalika wanamafungo kurudi na kufanya rejea kwenye mizizi ya maisha na utume wao kwa kujikita katika tafakari ya Neno la Mungu linalomwilishwa katika maisha na utume wao.

Amewaonesha jiografia ya maisha ya Nabii Eliya, mwenzi mwema wa hija ya maisha ya kiroho katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, tayari kujitakasa mbele ya Mungu, ili kuendelea na dhamana ambayo wamekabidhiwa na Mama Kanisa. Wanapaswa kuelekeza mapambano yao dhidi ya uchu wa madaraka, ili kukazia mambo msingi katika maisha ya mwanadamu, kwa kutambua kwamba, katika ubinadamu wao, wanaweza kutumbukia katika kishawishi cha uchu wa madaraka.

Jiografia na mazingira ya Nabii Eliya, yalijikita katika muundo wa biashara, ulinzi na usalama pamoja na kilimo; mambo ambayo yalisaidia kuharakisha mchakato wa maendeleo ya wananchi wa Israeli. Hapa Waisraeli wakaonja raha na starehe, wakaanza kupoteza utambulisho wao wa kimaadili na kidini na hatimaye, wakamweka Mwenyezi Mungu ukutani kama picha ya mapambo. Mambo haya yalimkasirisha sana Nabii Eliya, akataka Mwenyezi Mungu awawashie cheche za moto, ili wakione cha mtema kuni!

Padre Secondin anasema, hapa Nabii Eliya alisahau kuwa ni Nabii ambaye alipaswa kusikiliza kwa makini na kutii na wala si kuwa badala ya Mwenyezi Mungu kwa kutoa amri na maagizo; matokeo yake, anabwaga manyanga na kukimbilia Jangwani katika hali ya upweke, ili kujitakasa na kujikita katika mizizi ya uaminifu kwa Mungu kwa kutambua kwamba, kweli hata maskini wanayo nguvu ya kuwainjilisha wenye nguvu kama Nabii Eliya anavyoshuhudia kwa kukutana na Mjane wa Serapta. Upendo na huruma ya Mungu, vipewe kipaumbele cha kwanza sanjari na kuendelea kujiaminisha na kuonesha utii kwa Mungu.

Padre Secondin anasema kwamba, Mwenyezi Mungu anazungumza mambo machache sana, kumbe, kuna haja ya kumsikiliza kwa umakini mkubwa, kwa kuonesha uvumilivu; ukweli na uwazi. Wanamafungo wametakiwa kujiuliza, Je, bado wana ari na upendo ule wa awali kwa Kristo na Kanisa lake? Wanajisadaka kwa ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, au wao ndio wanaotaka, kuheshimiwa, kuangaliwa na kuhudumiwa zaidi? Je, wanataka kupata mafanikio ya chapu chapu kwa kuchanganya mambo?

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.