Mashambulizi ya kigaidi yanayoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia, yanawajengea
watu hofu ya usalama wa maisha yao, kiasi hata cha kutothubutu kupanga safari za hija
kama ilivyokuwa hapo awali wakati wa Kipindi cha Pasaka. Lakini, watu hawana budi
kuvunjilia mbali woga usiokuwa na msingi, lakini pia vyombo vya ulinzi na usalama
kitaifa na kimataifa havina budi kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara, vinginevyo,
watu wachache wanaopandikiza mbegu ya chuki na hofu miongoni mwa jamii wanaweza kufanikisha
azma yao kama jamii haitakuwa makini kupambana nao kikamilifu.
Kwa sasa kuna
picha za propaganda zinazooneshwa kwenye mitandao ya kijamii kuonesha ukatili mkubwa
unaofanywa huko Mashariki ya kati, kiasi cha watu kubaki wakiwa wameshikwa bumbuwazi
kutokana na ukatili huu usiokuwa na chembe ya huruma! Viongozi wa Kanisa katika Nchi
Takatifu wanawaalika mahujaji na watu wenye mapenzi mema kutositisha kufanya hija
za maisha ya kiroho katika maeneo matakatifu, kwani hiki ni kielelezo cha ushuhuda
wa udugu na mshikamano wa kweli wakati wa raha na machungu.
Mahujaji katika
maeneo matakatifu wamekuwa ni vyombo vya matumaini kwa Wakristo huko Mashariki ya
Kati wanaoendelea kuteswa, kudhulumiwa na kunyanyaswa kutokana na imani yao kwa Kristo
na Kanisa lake. Mauaji ya kikatili na ukosefu wa ulinzi na usalama ni kati ya mambo
ambayo yanaendelea kuwatia shaka watu wengi kupanga safari ili kutembelea maeneo matakatifu
kwa kuhofia hatima ya maisha yao.
Lakini viongozi wa Kanisa wanasema kwamba,
Yerusalemu na Bethlehemu ni maeneo ambayo yako salama hadi sasa, kumbe, mahujaji hawana
haja ya kuwa na wasi wasi na kwamba, kuna mahujaji bado wanaendelea kufanya hija zao
kwenye Nchi Takatifu. Viongozi wa Kanisa wanawaalika kutembelea maeneo matakatifu
kwani ni salama.
Ili kusaidia mahujaji wasiokuwa na uwezo mkubwa kufanya hija
katika maeneo matakatifu, hususan vijana, Kanisa mjini Yerusalemu limeamua kuanzisha
kituo cha hija, ambacho hapo tarehe 17 Februari 2015, Patriaki Fouad Twal wa Yerusalem
alibariki jiwe lake la msingi, ili ujenzi uanze mara moja na kwamba, kitaitwa "Kituo
cha Hija cha Papa Francisko" na kinajengwa kwenye mji wa Beit Jala, karibu na mji
wa Bethlehemu. Kazi ya ujenzi inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2015, ili
vijana waweze kuanza kukitumia kituo hiki hapo mwakani.
Na Padre Richard A.
Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.