2015-02-23 14:36:56

Ziara ya Pinda mkoani Iringa!


Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amesema anakubaliana na ombi la wakazi wa Nyanzwa na Igunda wilayani Kilolo, mkoani Iringa kuhusu ujenzi wa bwawa la kuhifadhia maji yatakayovunwa msimu wa mvua ili yasaidie kuongeza eneo la mradi wa umwagiliaji. Ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati akiwahutubia wakazi wa vijiji vya Nyanzwa na Igunda, mara baada ya kukagua mradi wa umwagiliaji wa Nyanzwa ambao ni maarufu kwa kilimo cha vitunguu.

“Huu mradi ni wa siku nyingi. Nimewauliza wataalamu niliokwenda nao wakasema ujenzi wa bwawa ndiyo suluhisho pekee la kuokoa mradi huu na kwamba ni jambo linalowezekana kama fedha zipo.” Aliutaka uongozi wa mkoa uandae mpango kazi na wauweke kwenye bajeti ya mwaka ujao wa fedha ili mradi huo uweze kuombewa fedha kwenye bajeti kuu ya Serikali. ia aliwataka wakazi wa eneo hilo wakitunze chanzo cha maji kwa kuweka mipaka ili watu wasikivamie na hatimaye kukiharibu.

“Tengeni eneo kwa kuweka mipaka. Mkurugenzi simamia uwekaji wa mipaka kwenye chanzo hiki ili tukilinde kwani uharibifu wa mazingira utakiharibu kabisa,” alisisitiza. Akiwa katika ukaguzi wa eneo la mradi, Waziri Mkuu alikutana na mkulima mmoja wa vitunguu Bw. Furaha Ngalali (32) ambaye alimweleza kwamba mwaka jana alifanikiwa kulima ekari tatu za vitunguu ambazo zilimpatia kiasi cha milioni 6/- huku kila gunia akiwa ameliuza kwa sh. 70,000/-.

“Gharama kwa kila ekari ni karibu sh. 600,000/- kwa hiyo kwa ekari tatu ni sh. milioni 1.8/-. Tukivuna vitunguu tunaandaa bustani ya mbegu na pia humu tunapanda maharage,” alisema Bw. Ngalali alpoulizwa Waziri Mkuu analima eneo hilo mara ngapi kwa mwaka. Alipoulizwa soko la vitunguu wanapata wapi, Bw. Ngalali alisema wanunuzi huwa wanavifuata huko huko Nyanzwa na kwamba wengi wao hutoka Dar es Salaam, Mbeya na Songea. Kijiji cha Nyanzwa kipo umbali wa kilometa 36 kutoka Ruaha Mbuyuni ilipo barabara kuu ya kuelekea Dar es Salaam na Mbeya.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wakazi wa vijiji vya Nyanzwa na Igunda wajikite kwenye ufugaji wa nyuki kwani hauna gharama kubwa na unawawezesha wananchi kuinua kipato chao kwa haraka. “Wakati mkisubiri ujenzi wa bwawa ili muongeze uzalishaji wa mbogamboga ni vema mkaangalia suala la ufugaji nyuki… licha ya kutumika kama sehemu ya kujiingizia kipato, pia ufugaji nyuki ni njia mojawapo ya utunzaji wa misitu,” alisema.

“Hapa mlipo kuna msitu mkubwa wenye migunga na mibuyu mingi tu. Yote hii imechanua maua mengi mno. Lazima tutumie uwepo wa misitu hii kama fursa ya kipekee ya kujiingizia kipato kwa kuweka mizinga ya nyuki. Unaweza usipate mahindi au vitunguu lakini asali ikawasaidia kuwapa kipato. Hivi sasa lita moja ya asali imefikia sh. 15,000/- hadi sh. 20,000/- na tena mtapata nta ambayo pia ina bei nzuri tu,” alisema.

Alisema kwa sasa asali inauzwa kwa bei ghali kwenye nchi mbalimbali baada ya kuongezeka kwa mahitaji yake na hasa ikizingatiwa kwamba inatumika kama dawa ya kutibu magonjwa mbalimbali na pia kwenye baadhi ya vipodozi.

Mapema, akisoma taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mtendaji wa Kijiji cha Nyanzwa, Bw. Hekima Masanula alisema skimu ya umwagiliaji ya Nyanzwa ilijengwa mwaka 1960 wakati huo kwa kutumia banio la miti na magunia ya mchanga. Ilikuja kuboreshwa miaka ya 90 kwa ufadhili kutoka Jumuiya ya Ulaya na Serikali ya Sweden. “Hata hivyo, skimu hii ambayo inahudumia wakulima 3,469 wakiwemo wanaume 1,662 na wanawake 1,807; inakabiliwa na uhaba wa maji kwani ni hekta 256 tu ambazo zinamwagiliwa kwa sasa wakati eneo lote la mradi ni hekta 940,” alisema Bw. Masanula.

Alisisitiza ombi la kujengewa bwawa kama njia pekee ya kuwakwamua wakazi hao kutokanana shida ya maji inayowapata hasa wakati wa kiangazi.

Wakati huo huo Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameutaka uongozi wa mkoa wa Iringa uangalie uwezekano wa kuanzisha Halmashauri mpya katika wilaya ya Kilolo kata ya Mahenge na tarafa ya Mahenge kwa sababu ya hali ya kijiografia ya eneo hilo. “Makao makuu ya wilaya hii yako Kilolo kule milimani. Ukitaka kuja huku ni lazima upite kwanza mjini ndipo ufike huku. Hapana! Hatuwezi kuwasaidia wananchi hawa kujiletea maendeleo kwa staili hii,” alisema Waziri Mkuu.

Alikuwa akihutubia wakazi wa vijiji vya Nyanzwa na Igunda wilayani Kilolo, Jumamosi, Februari 21, 2015) mara baada ya kukagua mradi wa umwagiliaji wa Nyanzwa ambao ni maarufu kwa kilimo cha vitunguu. Vijiji hivyo viko umbali wa km. 120 kutoka Ipogoro ilipo njia panda ya kwenda Iringa mjini na km. 155 kutoka Kilolo mjini yalipo makao makuu ya wilaya hiyo.

Waziri Mkuu alisema kata za tarafa hiyo ni kubwa mno kwa mtendaji kuweza kusukuma maendeleo ya wananchi. “Kata hii imeanzia Kitonga hadi huku Nyanzwa. Hivi ni mtendaji gani anayeweza kuja kuhimiza shughuli za maendeleo akitokea huko?” alihoji Waziri Mkuu huku akishangiliwa. Alisema mbali na idadi ya watu, suala la kijiografia huwa linaangaliwa wakati wa kuanzisha maeneo ya utawala. “Hili eneo ni zuri, fursa zipo lakini linakosa usimamizi ndiyo maana hata wilaya hii inaongoza kwa umaskini kuliko wilaya nyingine za mkoa huu. Acheni wilaya ibaki moja, mbunge abaki mmoja lakini Halmashauri ziwe mbili ili muweze kusukuma maendeleo ya eneo hili kwa sababu mtakuwa na madiwani wenu na bajeti yenu,” alisema.

Mapema, akisoma taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mtendaji wa Kijiji cha Nyanzwa, Bw. Hekima Masanula Katemo alisema skimu ya umwagiliaji ya Nyanzwa ilijengwa mwaka 1960 wakati huo kwa kutumia banio la miti na magunia ya mchanga. Ilikuja kuboreshwa miaka ya 90 kwa ufadhili kutoka Jumuiya ya Ulaya na Serikali ya Sweden.

“Hata hivyo, skimu hii ambayo inahudumia wakulima 3,469 wakiwemo wanaume 1,662 na wanawake 1,807; inakabiliwa na uhaba wa maji kwani ni hekta 256 tu ambazo zinamwagiliwa kwa sasa wakati eneo lote la mradi ni hekta 940,”alisema Bw. Masanula.
Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake mkoani Iringa kwa kutembelea Manispaa ya Iringa ambako atakagua ujenzi wa maabara kwenye shule ya sekondari Kihesa, kuzindua kituo cha polisi cha Semtema, na kukagua huduma za afya kwenye hospitali ya manispaa ya iringa. Pia atakagua mradi wa machinjio ya kisasa ya Ngelewela kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara kwenye viwanja wa shule ya msingi Ipogolo.








All the contents on this site are copyrighted ©.