Baba Mtakatifu Francisko pamoja na wasaidizi wake wa karibu, Jumapili jioni tarehe
22 Februari 2015 wameanza mafungo ya maisha ya kiroho yanayoongozwa na Padre Bruno
Secondin, Jaalim mstaafu wa tasaufi mamboleo na maisha ya kiroho kutoka Chuo kikuu
cha Kipapa cha Gregorian, kilichoko mjini Roma. Mafungo haya yatakamilika hapo Ijumaa,
tarehe 27 Februari 2015.
Mafungo haya anasema Padre Bruno kutoka Shirika la
Wakarmeli kwamba, yanaongozwa na maneno ya Nabii Elia, moja ya Manabii wakuu wa Agano
la Kale, aliyeonesha uaminifu mkuu mbele ya Mwenyezi Mungu licha ya madhulumu na nyanyaso
alizokumbana nazo katika hija ya maisha yake hapa duniani. Akakimbilia Jangwani, ili
afunikwe na kifo, lakini huko akashibishwa na mkate wa ajabu na kuzima kiu yake kwa
maji yaliyotoka mwambani, kiasi hata cha kumwezesha kustahimili adha ya jangwani kwa
muda wa siku arobaini, hadi siku ile alipofanikiwa kuupanda Mlima wa Oreb na hatimaye,
akakutana na Mwenyezi Mungu, katika hali yake ya unyonge na udhaifu.
Padre
Bruno anasema mafungo haya ni changamoto ya kutaka kurejea tena katika mizizi ya maisha
ya kiroho, ili kuwa na ujasiri wa kukataa maisha ya undumilakuwili pamoja na kukumbatia
miungu wadogo wadogo badala yake kuwa na ibada ya kweli kwa kumwachia nafasi Mwenyezi
Mungu ili aweze kuwashangaza katika hali ya ukimya na kwamba, maskini wanayo nafasi
ya pekee katika kuwainjilisha Watu wa Mataifa. Kutokana na mantiki hii, Wakristo hawana
budi kuwa kweli ni mashuhuda wa haki na mshikamano; unabii na udugu.
Padre
Bruno anasema, tafakari zake zitaongozwa na maisha ya sala, ili kuwasaidia wahusika
kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Neno la Mungu ni chakula cha
maisha ya kiroho, ambacho utamu wake ni endelevu. Kipindi hiki cha Mafungo ya kiroho
kwa Baba Mtakatifu Francisko na wasaidizi wake wa karibu, hatafanyaKatekesi yake siku
ya jumatano na mazungumzo binafsi kwa sasa yamesitishwa hadi pale watakaporudi kutoka
Jangwani!