2015-02-23 08:42:07

Shirikisheni mawazo yenu kuhusu familia!


Kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia itakayofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba 2015, Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini limetuma maswali dodoso 42 kwenye mitandao ya kijamii ili kuwashirikisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutoa maoni, mawazo na tafakari kuhusu masuala kadhaa kuhusu maisha ya ndoa na familia, ili hatimaye, kuyafanyia kazi, tayari kuyawasilisha kwenye Sekretarieti kuu ya Sinodi mjini Vatican, tayari kwa ajili ya maandalizi ya hati ya kutendea haki, yaani “Instrumentum Laboris”.
Maswali haya dodoso yamechukuliwa kutoka kwenye Hati ya Mababa wa Sinodi maalum ya Maaskofu iliyofanyika mwezi Oktoba, 2014. Itakumbukwa kwamba, kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Sinodi ya maaskofu kuhusu familia ni “Wito na utume wa familia katika Kanisa na Ulimwengu mamboleo”. Maoni na mchango wa waamini na watu wenye mapenzi mema nchini Afrika ya Kusini, utawasaidia Maaskofu kuwa na mawazo mapana zaidi kuhusiana na halisi ya maisha na utume wa watu wa ndoa na familia.
Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini linapania kupata walau mwanga wa matatizo maalum yanayogusa maisha na utume wa familia nchini humo. Kutokana na sababu mbali mbali wanasema Maaskofu kuna familia ambazo kwa sasa zinaendeshwa na watoto wadogo. Waamini wanaweza kuwasilisha maoni yao hadi tarehe 27 Machi, siku chache kabla ya Maaskofu hawajawasilisha mawazo yao kwenye Sekretarieti kuu ya Sinodi ya Maaskofu hapo tarehe 15 Aprili 2015.
Taarifa zinaonesha kwamba, Kanisa Katoliki sehemu mbali mbali za dunia zimeamua kutuma maswali dodoso kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kwa njia ya mitandao ya kijamii, ili kupata mawazo ya wengi, licha ya utaratibu unaotumiwa na Kanisa katika kupata taarifa zake. Lakini itakumbukwa kwamba, kwa mara ya kwanza hata Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu ilichapisha maswali dodoso kwenye mtandao ili kuwapatia watu wengi zaidi kushiriki na matokeo yake yalikuwa kweli ni ya kushangaza.
Kumbe si bure, kuona watu wengi wanafuatia kwa kina na mapana maadhimisho ya Sinodi kwa ajili ya familia, kwani hapa ni kitovu cha maisha na matumaini ya binadamu kwa sasa na kwa siku za usoni.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.