2015-02-23 08:45:21

Serikali nchini Angola kushirikiana na Makanisa katika sekta ya elimu!


Baraza la Makanisa nchini Angola, CICA linaendelea kuimarisha mshikamano wa umoja na udugu kati ya Makanisa pamoja na Serikali katika sekta ya elimu na majundo makini kwa vijana wa kizazi kipya. Hizi ni juhudi zilizofanikishwa kati ya Bwana Manuel Vicente, Makamu wa Rais nchini Angola alipokutana na kuzungumza na viongozi wa Makanisa nchini humo.
Makamu wa Rais amekazia umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na Makanisa, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya vijana wa kizazi kipya nchini Angola, ili kuwajengea imani na matumaini mapya yatakayosaidia kukoleza mchakato wa maendeleo yao kiroho na kimwili, kwa kujikita pia katika utu wema na kanuni maadili, dhamana ambayo inaweza kutekelezwa barabara na viongozi wa kidini.
Mama Deodolinda Dorcas Tecas, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa nchini Angola amesema, Serikali inataka kuhakikisha kwamba, inaunganisha nguvu kwa kushirikiana na Makanisa katika mchakato wa maboresho ya elimu nchini humo. Lengo ni kusaidia kutoa elimu kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi; vijana wanaotumia dawa haramu za kulevya pamoja na kuendelea kuogelea katika ulevi wa kupindukia, jambo linalochangia ajali nyingi barabarani, ujambazi pamoja na uvunjifu wa misingi ya haki, amani na utulivu nchini Angola.
Baraza la Makanisa Angola kwa kushirikiana na Serikali litawekeza zaidi katika huduma kwa makundi haya ya vijana, ili kuyasaidia kugundua tena ndani mwao, kwamba, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, wanapendwa na kuthaminiwa na Kanisa na Jamii katika ujumla wao, kumbe ni wajibu wao kuenenda katika utu wema, kwa kuheshimu maisha, ambayo ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu. Makanisa yatafanya kazi bega kwa bega na Wizara ya elimu, familia, maendeleo ya wanawake pamoja na wizara ya utamaduni.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.