2015-02-23 09:16:11

Ni mapambano hadi kieleweke!


Kwaresima ni kipindi cha mapambano ya maisha ya kiroho dhidi ya Shetani na vishawishi vya dhambi; mapambano ambayo yanajikita katika toba na wongofu wa ndani. Ni changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 22 Februari 2015, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Anasema, mapambano dhidi ya Shetani na vishawishi vya dhambi yanahitaji muda, nafasi, ukimya na sala, ili kutambua nafasi ambazo Shetani anaweza kuzitumia ili kumwangusha chini mwamini, lakini akumbuke kwamba, kwa msaada na neema ya Mungu anaweza kushinda yote haya.

Baba Mtakatifu anasema, kuna haja ya kuwa na jangwa katika maisha, mahali pa salama na utulivu, kama jangwa ambalo Yesu anasimulia katika Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Kwaresima. Kule jangwani anasema Baba Mtakatifu Yesu alijitenga na malimwengu akaenda kusali kabla ya kuanza utume wake wa maisha ya hadhara. Akakaa huko kwa kipindi cha siku arobaini, akapambana uso kwa uso na Shetani na hatimaye akamshinda. Na kwa njia ya Yesu, Wakristo wamemshinda pia Shetani, lakini wanawajibu wa kuhakikisha kwamba, kila siku ya maisha yao wanaendeleza ushindi huu hadi kieleweke!

Mama Kanisa mwanzoni mwa Kipindi cha Kwaresima anawakumbusha watoto wake kuhusu fumbo la Ushindi wa Yesu dhidi ya Shetani, ili kupata mwelekeo, maana na mbinu za kupambana na Shetani katika maisha ya kiroho. Ukimya ni fursa makini inayomwezesha mwamini kusikiliza sauti ya Mungu ambayo wakati mwingine inaweza kumezwa na ile sauti ya Shetani. Jangwa ni mahali pa salama pa mwamini kuweza kuzama katika undani wa maisha yake na kuanza mchakato wa mapambano kati ya maisha na kifo. Baba Mtakatifu anawauliza waamini ni kwa njia gani wanasikiliza kwa makini sauti ya Mungu inayozungumza kutoka katika dhamiri zao nyofu?

Kwa namna ya pekee, mwamini anaweza kuisikiliza sauti ya Mungu kwa Neno lake, changamoto na mwaliko kwa waamini kulifahamu Neno la Mungu, ili kukabiliana na Shetani kwa umakini mkuu, vinginevyo, mwamini anaweza kukiona cha mtema kuni. Waamini wajenge utamaduni wa kusoma na kulitafakari Neno la Mungu kila siku ya maisha yao. Jangwa na Kwaresima linawasaidia waamini kushinda kishawishi cha kutaka kumezwa na malimwengu na miungu wadogo wadogo; linawasaidia kufanya maamuzi thabiti mintarafu Injili, upendo na mshikamano na jirani.

Kabla ya Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu amewaomba waamini kuwasindikiza wakati huu wanapoendelea na mafungo yao ya maisha ya kiroho, yanayowahusisha Baba Mtakatifu pamoja na wasaidizi wake wa karibu. Kipindi hiki cha kujichimbia jangwani, kiwasaidie kusikiliza kwa makini sauti ya Yesu na kuanza mchakato wa kusahihisha na kurekebisha mapungufu yao binafsi pamoja na kupambana kufa na kupona na vishawishi vinavyowakabili kila siku ya maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.









All the contents on this site are copyrighted ©.