2015-02-23 08:32:50

Ni kipindi cha neema na baraka!


Imekwishagota miaka 10 tangu Mtumishi wa Mungu Padre Luigi Giussani alipofariki dunia na miaka 60 tangu alipoanzisha Jumuiya ya Umoja na Uhuru. Sehemu mbali mbali za dunia zinafanya kumbu kumbu hii kwa njia ya Ibada ya Misa takatifu. Tarehe 23 Februari 2015, Kardinali Angelo Scola, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Milano, ameadhimisha kumbu kumbu hii kama alivyofanya Kardinali Agostino Vallini kwa Jimbo kuu la Roma.
Kardinali Mario Poli, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Buenos Aires ataadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa ajili ya kumbu kumbu hii hapo tarehe 26 Februari 2015. Wanajumuiya wa Umoja na Uhuru watafanya maadhimisho ya kimataifa hapo tarehe 7 Machi 2015 kwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican.
Padre Julian Carron, Rais wa Jumuiya ya Umoja na Uhuru katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha kwamba, hiki ni kipindi cha neema na baraka na kadiri muda unavyozidi kuyoyoma ndivyo wanavyogundua utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho na kiutu ulioachwa na Mtumishi wa Mungu Padre Luigi Giussani. Ni kiongozi aliyebahatika kuwa na karama, mwono wa mbali na tafakari ya kina kuhusu Ukristo na mchango wake katika ustawi na maendeleo ya binadamu: kiroho na kimwili.
Kardinali Joseph Ratzinger wakati huo, alipokuwa anaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya mazishi ya Mtumishi wa Mungu Luigi Giussani alikazia kwamba, Ukristo si dini inayojikita tu katika muundo wa mafundisho sadikifu, kanuni maadili, bali ni mchakato wa kutaka kukutana na Yesu Kristo katika hija ya maisha ya mwanadamu, ili kumtolea ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kama alivyofanya Mtumishi wa Mungu Luigi Giussani.
Ukristo unamwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu, ili kuwaonjesha ile furaha, mapendo, huruma na imani inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Ushuhuda wenye mvuto unashinda yote, kwani hapa mwamini anaalikwa kwa namna ya pekee kumwangalia Yesu Kristo Mkombozi wa dunia, ili kuweza kuwashirikisha na kuwamegea wengine ile Injili ya Furaha kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo.
Ni changamoto inayowasukuma, waamini kutoka katika undani wa maisha yao, ili kuwaendea maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, tayari kuwashirikisha utajiri ambao wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kanisa.
Padre Julian Carron anasema, tayari wamekwishajiandaa kukutana na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko, kwa ajili ya kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa ajili ya uwepo wa Mtumishi wa Mungu Padre Luigi Giussani. Wanasubiri kwa hamu, kusikiliza changamoto, dira na mwongozo kutoka kwa Baba Mtakatifu, utakaowawezesha kuendelea kumwilisha karama ya Mtumishi wa Mungu Luigi Giussani, kwa uaminifu na mapendo makuu.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.