2015-02-23 11:07:02

Nenda ukawaambie...!


Mpendwa msikilizaji wa kipindi chetu cha Kanisa la Nyumbani, Tumsifu Yesu Kristo! RealAudioMP3
Tukiwa ndani ya Kipindi cha Kwaresma ambapo Mama Kanisa anatualika sote kushughulikia wongofu wetu binafsi kwa namna ya pekee, tunaendelea kujitafiti, kujitathimini, kujikosoa, kujirekebisha ili tuweze, kujitakasa, kujijenga upya, kujiimarisha katika imani, maisha adilifu na uwajibikaji wa kweli katika nyanja mbalimbali za maisha, ili kwa utumishi wetu wa daima, Kanisa lisonge mbele, tuendelee kuijenga na kuilinda familia ya Mwanadamu kwa sifa na utukufu wa Mungu na kwa wokovu wetu.

Kukukumbusha tu mpendwa msikilizaji, tumekuwa katika safari ndefu na nzuri sana ya kuzipitia hati za Mtaguso Mkuu wa II wa Vatican. Kwa kumbukumbu ya daima, Mtaguso huo ulitoa jumla ya hati 16, ndanimwe zikiwemo Katiba nne, maagizo tisa na matamko matatu. Tumekwishakupitia hati kumi na tano hadi sasa, ambazo zimetukumbusha na kutuchangamotisha juu ya asili na utume wa Kanisa, na juu ya wajibu wetu sisi kama Wanakanisa. Lengo letu katika kufanya hivi, ni kujipatia ule uwezo wa kufikiri na kutenda pamoja na Kanisa.

Ni jukumu letu sote tunaomsadiki Kristo, kulifanya Kanisa lizidi kuwa hai katika uwepo wake, katika mafundisho yake na utume wake. Mtaguso Mkuu wa II wa Vatikani unatujenga kwa namna hiyo. Na kila mmoja akishakukumbushwa na kujengeka kwa mafundisho haya ya Mama Kanisa, anatumwa kuwaendea watu wote ili kuwatangazia Upendo wa Mungu na Injili ya furaha. Ndiyo maana leo tunafunga kitabu cha tafakari za hati za Mtaguso Mkuu wa II wa Vatican kwa kutafakari hati hii ya mwisho, kwa kilatini ikijulikana kwa jina la Ad gentes, ikiwa na maana kwa mataifa! Katika makala haya tunapenda kukushirikisha kwa muhtasari yale ambayo tumejifunza hadi sasa. Baada ya kukumbushwa yote ambayo Mama Kanisa alitupatia kwa njia ya Mtaguso Mkuu wa II wa Vatican, sasa ndugu msikilizaji unatumwa leo, nenda!! Wapi?? Kwa mataifa. Ukafanye nini kwa mataifa?? Sikia!

Nenda kwa Mataifa, Ukawakumbushe Upendo wa Mungu unayomwilika katika Kanisa kama Mwanga wa Mataifa (hilo tumejifunza katika hati ile iitwayo Lumen gentium yaani Mwanga wa mataifa, inayohusu fumbo la Kanisa). Ukawakumbushe hadhi na Ukuu wa Mungu anayepaswa kuabudiwa kwa Ibada takatifu na kamilifu (Hilo tumelikuta katika Katiba ile iitwayo Sacrosanctum concilium, yaani mkutano mtakatifu, inayohusu Liturujia Takatifu). . Ukawakumbushe mataifa juu ya Mungu anayejifunua kwetu kwa njia ya Neno lake, tupende kuyasoma na kuyajifunza maandiko matakatifu, tujifunze mapokeo hai ya Kanisa, na mafundisho ya mamlaka-funzi ya Kanisa, ili tujue zaidi Mungu ni nani na anataka nini kwetu (hilo tumelikuta katika Katiba ile iitwayo Dei Verbum yaani Neno la Mungu, ihusuyo ufunuo wa Kimungu). Ukawakumbushe mataifa juu ya utume wa Kanisa katika Ulimwengu wa Kisasa (hilo tumelikuta katika katiba ile iitwayo Gaudium et Spes, yaani furaha na matumaini). Ukawakumbushe mataifa kuwa watumie mambo mema ya mawasiliano ya nyakati zetu kwa ajili ya kueneza utukufu wa Mungu na ujumbe wa wokovu wa mwanadamu kiroho na kimwili (hilo tumelikuta katika hati ile iitwayo Inter mirifica, yaani kati ya mambo ya kushangaza, hati ihusuyo vyombo vya upashanaji habari).

Ukawakumbushe mataifa kuwa pamoja na tofauti zetu tulizonazo, sisi sote ni watoto wa Baba Mmoja, ambaye ni Mungu. Tujibidishe zaidi kujenga umoja kuliko kuabudu mitengano yetu, kwani ni kashfa kwa mataifa (hilo tumelikuta katika hati ile iitwayo Unitatis redintegratio yaani urudishaji wa umoja, hati ihusuyo mambo ya Uekumene). Ukawakumbushe Kanisa ni mmoja, takatifu katoliki la mitume, na Kristo ndiye kichwa cha Kanisa, anapenda nasi tuwe kitu kimoja. Tushirikiane katika yale yatuunganishayo kwa ajili ya wokovu wa roho zetu (hilo tumelikuta katika hati ile iitwayo Orientalium ecclesiarum, ihusuyo Makanisa Katoliki ya mashariki). Ukawakumbushe mataifa kwamba, daima tunaitwa kuwa kundi mmoja, na waangalizi wetu wakuu ni Maaskofu wetu, walio waangalizi wakuu wa imani katika makanisa mahalia, tuwape ushirikiano, tuwatii, ili sauti yao ituongoze tufike mbinguni (hilo tumejifunza katika hati ile iitwayo Christus Dominus, yaani Kristo Bwana, inayohusu huduma ya Kichungaji ya maaskofu).

Ukawakumbushe mataifa kuwa, tunapaswa kumpenda Mungu na kujiweka wakfu kwa Mungu na jirani kwa mapendo makamilifu (hilo tumelikuta katika hati ile iitwayo Perfectae caritate, yaani mapendo kamili). Ukawakumbushe mataifa kwamba, ili kazi ya uinjilishaji isonge mbele, tunahitaji watenda kazi, hivyo tukoleze miito, tuwalee vizuri sana tena kwa upendo wa hali ya juu waseminari wetu (hilo tumelikuta katika hati ile iitwayo Optatam totius, yaani kuchagua yaliyo bora, hati ihusuyo ihusuyo malezi ya Kipadre).

Ukawakumbushe mataifa kwamba kila mkatoliki ana utume wa kutenda ndani ya Kanisa na katika jamii anamoishi. Utume huo unamwilika mahali popote kwa njia ya maisha ya ushuhuda wa imani na mapendo kwa watu wote (Hilo tumelikuta katika hati ile iitwayo Apostolicam actuositatem, yaani utendaji wa kitume, hati ihusuyo utume wa walei). Ukawakumbushe mataifa kukimbilia daima huruma ya Mungu, inayotolewa kwa njia ya mapadre wetu, ambao ni wanenaji wa siri za Kristo na waadhimishaji wa mafumbo ya Mungu. Tena uwaambie vizuri mataifa wajitahidi kuwatunza sana mapadre wao, ni mikono tendaji ya Kristo mwenyewe, ni Kristo mwingine (Hilo tumelikuta katika hati ile iitwayo Presbyterorum ordinis, ihusuyo huduma na maisha ya Kipadri).

Nenda kwa mataifa, ukawafundishe juu ya uzito wa malezi ya mwanadamu mkamilifu, kiroho, kiakili, kijamii, kimaadili, kiutashi. Uwaambie mataifa kwamba, aina ya watu tunaokuwepo ulimwenguni na vitimbwi tunavyofanya sasa, ni matokeo ya aina ya malezi tuliyopata. Tukitaka kizazi bora cha binadamu, tusipuuzie suala la malezi unganifu. Ukitaka kuwa na watoto wazuri, walee vizuri katika nyanja zote (hili tumelipata katika hati ile iitwayo Grafissimum educationis, yaaani uzito wa malezi).

Ukawakumbushe mataifa kwamba tuwapende na kuwatendea mema watu wote, sio wale wa imani yetu tu (Hili tumelipitia katika hati ile iitwayo Nostra aetate, yaani katika wakati wetu, tamko kuhusu uhusiano wa Kanisa na dini zisizo za Kikristo). Ukawakumbushe mataifa kuwa ni haki ya kila mwanadamu kumwamini Mungu na kumwabudu katika namna sahihi inatunza heshima ya Jina la Mungu na inayoheshimu uhai wa mwanadamu (Hili tulifundishwa katika tamko lile lililoitwa Dignitatis humanae, yaani Hadhi ya Mwanadamu).

Mpendwa msikilizaji, unatumwa na Mama Kanisa, nenda kwa mataifa! Hao mataifa ni nani?? Ni jirani yako, rafiki yako, adui yako, mfanyakazi mwenzako, bosi wako, familia yako, jumuiya yako, parokia yako, jimbo lako, taifa lako, kila huyo, hao wote ndio ‘mataifa’. Anza na huyohuyo aliyeko moyoni mwako, aliyeko pembeni yako, uliye naye ofisini, unayesafiri naye huyo, huyo anaye kutazama muda huu, huyo anayepita hapo mbele yako, huyo aliye mgonjwa kitandani. Hao ndio mataifa, wape ujumbe wa Mungu, uwaimarishe katika imani, matumaini na mapendo.

Nenda kwa mataifa, wewe ni mmisionari kuanzia hapohapo ulipo, sio lazima upande ndege au meli kwenda mbali sana. Hati hii ‘Ad gentes’, yaani kwa mataifa, ni hati inayobeba muhutasari wa mafundisho yoote ya Mtaguso Mkuu wa II wa Vaticani, ndiyo maana inakualika, baada ya kuyasikia hayo yote, usikae nayo peke yako, nenda kwa mataifa, ukawamegee nao. Ni hati inaeleza hulka ya kimisionari ya Kristo aliyetumwa na Baba ulimwenguni, na Kristo huyo anamwilika Katika tabia ya kimisionari ya Kanisa. Na sisi wanakanisa wote, tuwe wamisionari hai. Twende, kwa Mataifa!

Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB, mtawa Mbenediktini Mmisionari.








All the contents on this site are copyrighted ©.