2015-02-23 14:50:28

Malipo kwa wakulima Tanzania


Serikali ya Tanzania imepata mkopo wa sh. bilioni 15 ambazo zitatumika kulipa kiasi cha madeni ya mazao ya nafaka ambayo wakulima wanaidai kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA). Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Iringa akiwa kwenye ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo katika mkoa huo.

Akizungumza na wananchi mara baada ya kukagua Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo (SACCOS) cha Mazombe kilichopo Ilula wilayani Kilolo, mwishoni mwa wiki, Waziri Mkuu alisema katika kipindi cha mwezi huu, Serikali imepata mkopo huo kutoka benki ya CRDB ambazo zimesambazwa kwenye mikoa mbalimbali ili kuwalipa wakulima hao.

Alisema hadi kufikia Machi mwaka huu, Serikali itahakikisha inamaliza kulipa madeni kwa wakulima ambao waliuza mazao yao kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA). Akifafanua kuhusu mgao wa fedha hizo, Waziri Mkuu alisema kanda ya Arusha wamepata sh. bilioni 1.72/-; kanda ya Dodoma sh. bilioni 2.02/-; kanda ya Kipawa sh. milioni 632.3/-; kanda ya Makambako sh. bilioni 4.58/-; kanda ya Shinyanga sh. milioni 238.85/-; kanda ya Songea sh. bilioni 1.97/- na kanda ya Sumbawanga sh. bilioni 3.82/-.

Alisema fedha hizo zimegawanywa kwenye vituo, vikundi na mawakala na kuongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika itatoa sh. bilioni 15 nyingine ili zigawanywe katika kanda na kumaliza kabisa madeni ya wakulima. Alitoa ufafanuzi huo baada kutolewa malalamiko kuwa ucheleweshwaji wa malipo hayo kwa wakulima umewafanya baadhi yao washindwe kurejesha mikopo kwenye taasisi za fedha kwa wakati.

Alisema ucheleweshwaji wa malipo hayo ulitokana na ziada ya chakula kwenye msimu wa kilimo wa mwaka 2014 kuongezeka kwa kufikia zaidi ya tani milioni 1.3, ukilinganisha na ziada ya tani 300,000 za msimu uliopita. “Serikali ililazimika kununua mazao ya wakulima zaidi ya malengo yake… matokeo hayo mazuri ya kilimo, yalitokana na msisitizo wa Serikali kuwekeza kwenye pembejeo, mbegu bora pamoja na kuingiza nchini matrekta zaidi ya 1600.

Mapema, akisoma taarifa ya chama hicho mbele ya Waziri Mkuu, Mwenyekiti wa Mazombe SACCOS, Bw. Yohanes Mwemtsi, alisema kucheleweshwa kwa marejesho ya mikopo iliyochukuliwa na wakulima kunazorotesha maendeleo ya SACCOS hiyo kwa kushindwa kujiimarisha kimtaji. Alisema licha ya changamoto hiyo, chama hicho kimeshatoa mikopo yenye thamani ya sh. bilioni 4.3 kwa wanachama wake zaidi ya 1,300 huku kukiwa na ongezeko la wanachama wapya kwa wastani wa asilimia 10 kila mwaka.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda amemtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, Bw. Ahmed Sawa akae pamoja na Afisa Elimu wake na kuwapunguza walimu 230 waliozidi mahitaji ya walimu kwenye manispaa hiyo na badala yake wawapangie kwenda vijijini. Ametoa agizo hilo Jumapili, Februari 22, 2015, wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa kata ya Ipogolo waliofika kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Ipogolo, nje kidogo ya Manispaa ya Iringa. “Manispaa inahitaji walimu 534 lakini waliopo ni 764. Hapa kuna ziada ya walimu 230 tena kw shuke za msingi... Mkurugenzi kaa na Afisa elimu wako muwaondoe walimu waliozidi na kuwapangia waende vijijini ambako kuna mahitaji zaidi,” alisema.

“Kwa upande wa shule binafsi nako pia tatizo ni lile lile. Walimu wamezidi. Mahitaji ni walimu 75 waliopo ni walimu 142 ... wanaozidi ni walimu 67,” alisema Waziri Mkuu. “Sina tatizo na walimu wa shule binafsi kwa sababu wao wana mfumo wao wa ajira lakini hawa wa shule za Serikali ni lazima muwaondoe tena haraka sana. Waondoeni waende vijijini kwenye mahitaji makubwa sababu ualimu ni ualimu tu, siyo lazima mtu awe mjini ndiyo afundishe vizuri,” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliupongeza uongozi wa mkoa wa Iringa kwa kuwa na ufaulu wa juu kwenye shule za msingi lakini akawataka wajiulize ni kwa nini ufaulu huo umeanza kushuka tangu mwaka 2013. “Mwaka 2010 kiwango cha ufaulu kilikuwa asilimia 77; mwaka 2011 kilikuwa asilimia 87; mwaka 2012 kilipanda na kufikia asilimia 97. Lakini mwaka 2013 kilishuka hadi asilimia 82 na mwaka jana ni kama kipo palepale kwani kilikuwa asilimia 82.5. Kaeni mjiulize kumetokea nini na mtafanya nini ili kurudi tena kwenye asilimia 97 au zaidi.”

Akizungumzia suala la afya, aliwaeleza wananchi hao kwamba ameuagiza uongozi wa mkoa kupitia watoa tiba wake waweke utaratibu wa kutoa elimu walau kila baada ya miezi miwili au mitatu ili wananchi wapate ufahamu wa magonjwa makuu yanayosumbua hivi sasa. Akifafanua magonjwa ya akinamama, Waziri Mkuu aliyataja magonjwa hayo kuwa ni saratani ya matiti, saratani ya shingo ya uzazi na tatizo la fistula wakati kwa upande wa akinababa alisema wao wanahitaji kupatiwa elimu zaidi kuhusu ugonjwa wa tezi dume.

“Matatizo haya yanatibika lakini ni lazima watu waeleweshwe kwamba wakiwahi kwenda hospitali matatizo haya yanatibika lakini wakichelewa inakuwa tatizo zaidi,” alisema.








All the contents on this site are copyrighted ©.