Askofu mkuu Robert Ndlovu wa Jimbo kuu la Harare, Zimbabwe katika barua yake ya kichungaji
wakati huu wa Kwaresima anawataka waamini kuwakumbuka, kuwasaidia na kuwahudumia wagonjwa
kwa moyo wa upendo na ukarimu, kwa kutambua kwamba, Kwaresima ni kipindi cha toba
na wongofu wa ndani, kinachojikita katika matendo ya huruma. Ni wakati muafaka wa
kuikimbia dhambi na nafasi zake, ili kushikamana na kuandamana na Mwenyezi Mungu,
mwingi wa huruma na mapendo.
Kwaresima, iwasaidie waamini kuonesha mshikamano
wa pekee na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na
sababu mbali mbali za maisha; hawa ni watu ambao hata wakati mwingine, wanapewa kisogo
na Kanisa.
Askofu mkuu Ndlovu anasema, Kanisa halina mbadala katika kutoa huduma
hasa kwa wagonjwa na maskini. Hawa ni watu ambao wanateseka kiroho na kimwili, kumbe
kuna haja kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwasaidia na kuwahudumia kwa
upendo na huruma, kwani hii ni sehemu muhimu sana ya shughuli na mikakati ya kichungaji
inayotekelezwa na Mama Kanisa ambalo bado linapenda kuwekeza katika sekta ya elimu
na majiundo makini ya binadamu: kiroho na kimwili.
Kanisa limeendelea kuwa
mstari wa mbele kwa kuwasaidia waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi; watoto yatima na wale
wote wanaoishi katika mazingira hatarishi na kwamba, Kanisa pia linachangia katika
tafiti mbali mbali zinazolenga kuleta mabadiliko katika maisha ya watu. Huduma ya
afya inayotolewa na Mama Kanisa haina budi kumsaidia mtu mzima: kiroho na kimwili,
ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu kama anavyosema Kristo mwenyewe "nilikuwa
mgonjwa, ukaja kunitazama na kuhudimia". Kile ambacho waamini wanajinyima kama sehemu
ya sadaka na mfungo wao wa Kwaresima kiwasaidie wagonjwa kupata tiba muafaka mahali
walipo.
Baba Mtakatifu Francisko katika Ujumbe wake wa Kwaresima anawahamasisha
waamini kujenga na kuimarisha mshikamano wa upendo na udugu, kwa njia ya huduma makini
kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni mwaliko wa kuachana na
utandawazi usioguswa wala kujali mateso na mahangaiko ya wagonjwa. Sadaka ya Kwaresima
kwa mwaka huu Jimbo kuu la Harare, Zimbabwe itatumika kwa ajili ya maboresho ya huduma
ya afya Jimboni humo. Askofu mkuu Robert Ndlovu anawaalika waamini na watu wote wenye
mapenzi mema kusali na kuwaombea wagonjwa bila kusahau kuwahudumia kwa moyo wa huruma
na upendo!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio
Vatican.