Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amepiga marufuku ukarabati wa maabara za shule
za sekondari na kusisitiza kwamba ni lazima zijengwe mpya kama ambavyo Serikali
ilielekeza. Ametoa agizo hilo Jumamosi, Februari 21, 2015, wakati akizungumza na
mamia ya wakazi wa kata ya Ilula, mara baada ya kukagua ukarabati wa maabara za sayansi
kwenye shule ya sekondari Ilula, wilayani Kilolo, mkoani Iringa.
“Mmefanya
ukarabati kwenye jengo lililojengwa zaidi ya miaka 20 iliyopita. Kuna chumba nimekuta
ni kidogo mno sababu hakiendani na maelekezo sasa... chumba kimoja kimepasuka ukuta,
hapana! RC kama kuna nyingine ya aina hii kazi isiendelee,” alisema. “Huu ukarabati
mliofanya ni kinyume na maelekezo ya Serikali ya kutaka zijengwe maabara mpya. Tulisema
zijengwe maabara mpya ili ziweze kudumu kwa miaka mingi kidogo. Kuna chumba ceiling
board iko chini kwasababu ujenzi ni wa zamani. Ujenzi wa sasa mapaa yako juu zaidi
ili kuruhusu hewa ya kutosha,” aliongeza.
“Ningeweza kusema vunjavunja
lakini haitakuwa haki kwa sababu kuna fedha za watu zimetumika... kwa sasa yatatuhifadhi
kwa muda kidogo, lakini haya majengo hayatadumu hata kidogo,” alisema. Waziri Mkuu
pia alikataa kuahidi mchango aliiombwa achangie na kuwaeleza kwamba atakuwa tayari
kuchangia ujenzi wa jengo jipya na siyo ukarabati kwani huo utakuwa ni upotevu wa
fedha. Majengo aliyoonyeshwa Waziri Mkuu Pinda yalijengwa mwaka 1995 na yalikuwa yakitumika
kama maabara kwenye sekondari hiyo.
Alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Bibi
Amina Masenza asimamie watu wake ili ujenzi wa maabara uweze kukamilika kwa muda
uliopangwa. Mkoa huounahitaji mabaara 72 na zilizokamilika ni maabara tano tu huku
nyingine 53 zikiwa kwenye hatua mbalimbali za ujenzi na 13 bado zikokwenye msingi
na moja iko kwenye linta.
Mapema, akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu,
Mtendaji wa Kata ya Ilula, Bw. Titus Katemo alisema shule ya sekondari Ilula ilijenga
maabara zake mwaka 1995 kwa nguvu za wananchi na kwamba zilikuwa zikitumika toka kipindi
chote hicho. Alisema ili kuendana na matakwa ya Wilaya, ukarabati wa vyumba vitatu
ulianza Novemba 15, mwaka jana kutokana na vyumba hivyo kutumiwa nawatahiniwa wa kidato
cha nne wa mwaka 2014 kwenye mitihani ya vitendo.
“Makisio ya gharama za ukarabati
wa vyumba vitatu yalikuwa ni sh. 38,294,775.00 na tunatarajia ukarabati utakamilika
ifikapo tarehe 30 Machi 2015,” alisema na kumuomba Waziri Mkuu awasaidie awaunge mkono
kwa mchango kwani kasi ya wananchi kuchangia imekuwa ndogo. Waziri Mkuu anaendelea
na ziara yake wilayani Kilolo na mchana huu anaenda kukagua mradi wa umwagiliaji wa
Nyanzwa na pia atazungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara.