2015-02-21 11:12:37

Ni zamu ya Rais JK


Tanzania inaunga mkono kwa dhati Ushirikiano wa Kikanda na ni muumini mkubwa wa Umoja wa Afrika na Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema hayo Ijumaa tarehe 20 Februari 2015 jijini Nairobi mara baada ya kukabidhiwa uenyekiti wa EAC na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ambaye amekua mwenyekiti wa Jumuiya hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita.


"Tunaamini kwamba Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyogawanyika, haitaweza kuchukua nafasi yake kamili na heshima katika familia ya Mataifa ya Afrika na dunia kwa ujumla" Rais amesema na kuongeza kuwa Tanzania inakua kuwa masoko yaliyogawanyika, miundombinu hafifu baina ya nchi, havina nafasi katika dunia ya leo wala ya baadaye.

Rais Kikwete amesema na kumpongeza Rais Kenyatta kwa kusimamia utekelezwaji wa maazimio na miradi ya pamoja ya Jumuiya wakati wa kipindi chake cha uenyekiti na kuahidi kuwa Tanzania haitawaangusha wana Afrika Mashariki katika kutekeleza azma yao ya pamoja ya kuendeleza Jumuiya ambayo inaundwa na nchi za Burundi, Kenya, Rwanda, Tanzania na Uganda.

Rais Kikwete amesema katika utekelezaji wa ajenda ya EAC,biashara imeongezeka kwa kiasi kikubwa na kwamba nchi zote wanachama zinayaona matunda hayo. Katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2013 biashara katika nchi za EAC imeongezeka kutoka dola za kimarekani 3, 722.9 hadi dola 5,805.6 ambapo kati ya mwaka 2012 hadi 2013 kumekua na ongezeko la asilimia 6%

"Kama biashara isiyo rasmi ingerasimishwa, kwa hakika, ongezeko hili la biashara lingekua juu zaidi ya hapa, hivyo imefikia wakati muafaka kurasimisha biashara isiyo rasmi katika ushirikiano wetu" Rais amesema na kuongeza kuwa " kwa njia hii serikali zitakusanya kodi na hivyo kuna umuhimu wa kuelekeza nguvu katika kusaidia biashara ndogo ndogo na zile zisizo rasmi kwa kuziwekea mazingira mazuri".

Rais Kikwete amerejea nyumbani mara baada ya mkutano huo ambao umehudhuriwa na Marais wa nchi zote tano za Jumuiya na Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini ambaye amehudhuria kama mualikwa maalum katika kipindi hiki ambapo mazungumzo ya awali ya kuijadili nchi yake kama inaweza kupata uanachama katika EAC yanaendelea.








All the contents on this site are copyrighted ©.