Viongozi watendaji wa Mfuko wa Akiba ya Uzeeni wa Vatican katika kikao chake kilichohitimishwa
hivi karibuni unasema kwamba, habari zilizokuwa zimezagaa kwenye baadhi ya vyombo
vya habari kuhusu ukata ulioukumba Mfuko huu kiasi hata cha kushindwa kutekeleza dhamana
na majukumu yake kwa siku za usoni, si kweli ni uzushi mtupu.
Taarifa ya fedha
iliyopitishwa na Sekretarieti kuu ya Vatican inaonesha kwamba, hali ni nzuri na wala
hakuna sababu kwa wafanyakazi wa Vatican kuhofia malipo yao ya uzeeni kwa siku za
usoni. Taarifa ya fedha imepitiwa na kuthibitishwa pia na Baraza la Mfuko wa Akiba
ya Uzeeni wa Vatican inaonesha kwamba, kumekuwepo na ongezeko la mchango wa wafanyakazi
kwa asilimia 26% hata baada ya kuongeza muda wa miaka miwili kwa wafanyakazi kwenda
pensheni, yaani wafikiapo miaka 67 kwa wafanyakazi walei na kwa Wakleri na Watawa
wafikiapo miaka 72.
Takwimu zinaonesha kwamba, hali ya mfuko ni nzuri na kwamba
una rasilimali ya kutosha kuweza kugharimia akiba ya uzeeni kwa wafanyakazi wa Vatican
wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma makini kwa Kanisa. Mfuko unaonesha kwamba,
unaweza kukabiliana na gharama za malipo kwa asilimia 95% na kwamba, pato la mfuko
linaendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka kutokana na faida inayopatikana kutoka kwenye
vitega uchumi vyake.
Taarifa inaonesha kwamba, kuanzia mwaka 1993 hadi mwaka
2013 kumekuwepo na ongezeko la Euro 22, 256, 196 kwa mwaka. Katika kipindi cha miaka
sita iliyopita kumekuwepo na ongezeko kutoka kiasi cha Euro 23, 583, 882 hadi kufikia
Euro 26, 866, 657, kiasi cha fedha kinachotosha kugharimia pensheni kwa wafanyakazi
wa Vatican kwa sasa.
Taarifa ya Mfuko wa akiba ya uzeeni inaonesha kwamba,
hadi kufikia tarehe 31 Desemba 2014 mfuko ulikuwa na rasilimali yenye thamani ya Euro
477, 668, 000 na kwamba, kwa mwaka 2015 kutakuwa na salio la Euro 27, 140, 000. Rasilimali
na vitega uchumi vyake vyote ni sawa na zaidi ya Euro millioni 504, hali inayoonesha
kwamba, Mfuko wa akiba ya uzeeni Vatican unaendelea kufanya vyema kwa kuzingatia kanuni
maadili, ukweli na uwazi.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili
ya Radio Vatican.