Mama Kanisa anaendelea kuadhimisha Mwaka wa Watawa Duniani kwa shughuli mbali mbali
ili kuonesha mchango wa watawa katika maisha na utume wa Kanisa, hasa wakati huu,
Kanisa linapoadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa
Vatican walipochapisha Waraka wa juu ya Upendo mkamilifu, Perfectae caritatae.
Ni
kipindi cha kuchambua na kujiwekea sera na mikakati ya kichungaji kwa ajili ya kuhamasisha
na kuendeleza miito mitakatifu ndani ya Kanisa kutokana na ukweli kwamba, kuna Mashirika
ya kitawa na kazi za kitume ambayo yako hoi kutokana na uhaba wa miito. Kwa kutambua
changamoto hizi, Shirikisho la Watawa Kitaifa kutoka Chicago, nchini Marekani ambalo
kwa zaidi ya miaka 27 limejielekeza katika kuhamasisha, kukuza na kuhudumia miito,
limeandaa kongamano la kimataifa litakaloanza kutimua vumbi mjini Roma kuanzia tarehe
23 hadi tarehe 27 Februari, 2015 kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani.
Lengo
la Kongamano hili ni kutaka kubadilishana: uzoefu na habari na kuabinisha mbinu na
mikakati inayoweza kutumiwa na Mashirika mbali mbali ya kitawa na kazi za kitume katika
kuhamasisha miito ya kitawa. Kongamaono hili litawashirikisha walezi na wakuu wa Mashirika
ya kitawa na kazi za kitume kutoka sehemu mbali mbali za dunia pamoja na baadhi ya
maafisa kutoka Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume.
Na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.