Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 21 Februari 2015 amekutana na kuzungumza
na Chansella Angela Merkel na ujumbe wake kutoka Ujerumani ambaye baadaye alifanya
mazungumzo pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana
na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano
wa kimataifa mjini Vatican
Baba Mtakatifu pamoja na mgeni wake wamezungumzia
masuala ya kimataifa na kikanda kwa kujielekeza zaidi katika mkutano wa wakuu wa Nchi
Saba tajiri duniani, maarufu kama G7 utakaofanyika nchini Ujerumani; mapambano dhidi
ya baa la njaa na umaskini; biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo pamoja
na haki za wanawake duniani.
Viongozi hawa wawili wameangalia kwa pamoja changamoto
zinazoendelea kuikabili Jumuiya ya Kimataifa sanjari na utunzaji bora wa mazingira,
haki msingi za binadamu na uhuru wa kuabudu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kwa
kukazia umuhimu wa kudumisha tunu msingi za maisha ya kiroho kama nguzo ya maridhiano
na amani kati ya watu.
Baadaye Baba Mtakatifu na mgeni wake wamejikita zaidi
kuhusu hali ya Bara la Ulaya pamoja na kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Ulaya inajibidisha
zaidi ili kupata suluhu ya mgogoro wa vita nchini Ukraine.
Na Padre Richard
A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.