2015-02-21 16:31:13

Athari za mabadiliko ya tabianchi!


Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland katika Kampeni ya Kwaresima kwa mwaka 2015 linajielekeza zaidi katika kuwahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujifunga kibwebwe kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zimekuwa ni chanzo kikuu cha majanga sehemu mbali mbali za dunia.

Kuna baadhi ya nchi ambazo kwa sasa zinakabiliwa na ukame wa kutisha na kwa upande mwingine kuna nchi ambazo zinapambana na mafuriko ambayo yamesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao, kiasi hata cha kuwatumbukiza watu katika umaskini na magonjwa ya milipuko.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland linawaalika kwa namna ya pekee, waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuonesha mshikamano wa pekee katika kuchangia kwa hali na mali huduma zinazotolewa na Shirika la misaada la Kanisa Katoliki Ireland, Trocaire, ili kuwapatia watu huduma wanaokabiliwa na ukame wa kutisha huduma bora ya chakula na maji pamoja na kuwahakikishia kwamba, wanapata huduma ya afya.

Takwimu kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa zinaonesha kwamba, kila mwaka kuna watu zaidi ya 150, 000 wanaofariki dunia kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Katika kipindi cha Mwaka 2011, watu zaidi ya millioni kumi walishambuliwa kwa ukame wa kutisha. Mwaka 2013, tufani ya Hayan ilisababisha watu 6, 000 kufariki dunia nchini Ufilippini.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland linasema kwamba, mchango wa hali na mali ni muhimu sana katika kuwasaidia na kuwahudumia watu wanaopambana na athari za mabadiliko ya tabianchi sehemu mbali mbali za dunia. Shirika la Trocare lilianzishwa kunako mwaka 1973, leo hii linatekeleza dhamana na utume wake katika nchi 20 duniani, kwa njia ya huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; ni Shirika linalotetea haki msingi za binadamu pamoja na kuwahudumia wagonjwa wa Ukimwi bila kuwasahau wale wote wanaoteseka kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.