Mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Wakleri wa Jimbo kuu la Roma, Siku
ya Alhamisi, tarehe 19 Februari 2015 yamefanyika katika hali ya faragha, ili kumpatia
Baba Mtakatifu nafasi ya kuweza kuwafunda barabara Wakleri wenzake, ili waweze kuadhimisha
Mafumbo ya Kanisa kwa moyo wa ibada, ari na unyenyekevu mkuu, wakitambua kwamba, wao
wanayo dhamana ya kuwatangazia na kuwaadhimishia Watu wa Mungu, Mafumbo ya Kanisa.
Mapadre wanapaswa kuihudumia Familia ya Mungu kwa ukarimu na unyenyekevu mkuu
unaoshuhudiwa katika uhalisia wa maisha ya Wakleri wenyewe. Wakleri wa Roma wanamshukuru
Baba Mtakatifu kwa kuwapatia Waraka wake wa kichungaji wa Injili ya Furaha ambao kwa
sasa ni Mwongozo na dira ya mikakati na shughuli za kichungaji kwa Makanisa mahalia.
Ni Waraka unaohamasisha waamini kujisadaka kwa ajili ya kuwatangazia Watu
wa Mataifa Injili ya Furaha kwa njia ya ushuhuda wa maisha yanayomwilishwa katika
imani. Haya yamesemwa na Kardinali Agostino Vallini Makamu wa Askofu Jimbo kuu la
Roma wakati akimkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kuzungumza na Wakleri wa Jimbo
kuu la Roma, ili aweze kuwapatia changamoto zitakazowasaidia kuboresha mahubiri wakati
wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu.
Kardinali Vallini anasema, mahubiri
yasiyokuwa na mvuto wala mashiko kwa watu katika ukuaji wao wa maisha ya kiroho, yanachosha.
Wakleri ambao wanadhama ya kuhubiri Neno la Mungu walitaka kupata ushauri kutoka kwa
Baba Mtakatifu, ili uweze kuwasaidia katika mchakato wa maboresho ya mahubiri yao,
ili kuzima kiu na udadisi wa waamini wakati wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu.
Huu ni mchakato wa shughuli za kichungaji unaolenga kumsaidia Padre kuwa karibu zaidi
na Familia ya Mungu kwa njia ya mahubiri yanayomwilishwa katika maisha na vipaumbele
vyake.
Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa yapate chimbuko lake katika uhalisia
wa maisha yanayoshuhudia imani tendaji na ari ya kutaka kuwahudumia Watu wa Mungu
kwa kuwa na busara, ili kuwasaidia waamini katika hija ya maisha yao ya kiroho.
Na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.