Askofu mkuu mstaafu James Odongo, hapo tarehe 21 Februari 2015 ataadhimisha kilele
cha Jubilee ya Miaka 50 tangu alipowekwa wakfu kuwa Askofu, kwenye Kanisa kuu la Mashahidi
wa Uganda, Jimbo Katoliki la Tororo, Uganda na muda mfupi baadaye, akashiriki katika
maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican uliokuwa unaendelea mjini Vatican,
matendo makuu ya Mungu. Padre Joseph Healey, Mmissionari wa Maryknow ambaye kwa
miaka mingi ameishi na kufahnya utume wake katika Nchi za AMECEA, anasema, hadi wakati
huu, kuna Maaskofu watatu kutoka katika Nchi za AMECEA walioshiriki katika maadhimisho
ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, hawa ni pamoja na: Askofu mkuu mstaafu James Odongo,
Askofu mstaafu Colin Davies wa Jimbo Katoliki Ngong, Kenya pamoja na Askofu mstaafu
Gervas Placidus Nkalanga wa Jimbo Katoliki Bukoba ambaye kwa sasa anaendelea na maisha
ya sala na tafakari katika Monasteri ya Hanga, Jimbo kuu la Songea. Itakumbukwa
kwamba, Kikao cha nne na cha mwisho cha maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican,
kilijadili na kuchapisha nyaraka kumi na moja, kati ya nyaraka kumi na sita, zilizotolewa
na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican: Gaudium et spes; Neno la Mungu: Dei
Verbum, Fumbo la Kanisa, Lumen gentium; Ad gentes. Askofu mkuu mstaafu Odongo katika
mahojiano maalum na Padre Healey anasema kwamba, Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa
Vatican wote walitia mkwaju hati hizi, kwa ari na moyo wa mshikamano wa Kanisa, wakajiwekea
dhamana ya utekelezaji wa Mafundisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika Makanisa
mahalia. Padre Joseph Healey, mmissionari na mwandishi wa vitabu aliyebobea katika
tasnia ya habari, alikuwa ni Katibu wa kwanza wa Idara ya Habari, Shirikisho la Mabaraza
ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, yenye makao makuu yake, Jimbo
kuu la Nairobi, Kenya. Alibahatika pia kufanya kazi kwa karibu sana na Askofu mkuu
James Odongo, alipokuwa Mwenyekiti wa AMECEA kuanzia mwaka 1973 hadi mwaka 1979, umri
wa mtu mzima kabisa. Hapa ukawa ni mwanzo wa ujenzi wa Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo
kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa katika Nchi za AMECEA. Jumuiya ndogo
ndogo za Kikristo zikapania kuwa ni mahali pa kusoma na kulitafakari Neno la Mungu;
mahali pa kujiandaa kikamilifu katika maisha ya Kisakramenti sanjari na kumwilisha
imani katika matendo ya huruma. Mababa wa AMECEA walikazia pamoja na mambo mengine,
umuhimu wa Kanisa mahalia kujitegemea, kujiendeleza na kusimama kwa miguu yake. Kunako
mwaka 1974 hadi mwaka 1975 chini ya uongozi wa Askofu Vincent McCauley, ujenzi wa
Makao makuu ya AMECEA ukaanza Jijini Nairobi. Kunako mwaka 1975, AMECEA ikaanzisha
kozi maaum ya uhasibu, Chuo cha maendeleo ya jamii, Nyegezi, Jimbo kuu la Mwanza ambacho
kwa sasa ni Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino cha Tanzania, SAUT. Mwaka 1976, utume
kwa jamii za kichungaji ukaanzishwa na AMECEA. Historia inaonesha kwamba, Kanisa Katoliki
katika nchi za AMECEA linaendelea kuimarishwa kwa uwepo wa Jumuiya Ndogo ndogo za
Kikristo. Waswahili wanasema, usione vinaelea, kumbuka kwamba, vimeundwa! Na Padre
Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.