Tafakari ya Neno la Mungu JUMA LA 1 KWARESIMA, tunaongozwa na Neno la Mungu kama ifuatavyo!
Ingefaa hata wewe ndugu msomaji, ukavipitia vifungu hivi kama sehemu ya maadhimisho
ya Kipindi cha Kwaresima pamoja na kujitajirisha kwa Neno la Mungu, usiwe mtazamaji
tu! Mwa: 9:8-15 1Pt. 3:18-22 Mk. 1:12-15.
Tulipoanza
kipindi cha Kwaresima tulianza kwa kujipaka majivu – majivu ni alama na ukumbusho:Kama
alama - yatukumbusha mabaki – majivu yakitumika yaonesha masikitiko, shida, taabu
na toba. Angalia Ayubu – 42:6 alipopoteza kila kitu, alikaa juu ya majivu n.k. Majivu
hubaki baada ya moto kuunguza kila kitu. Baada ya dhambi ya asili kilichobaki ni dhambi.
Kama ukumbusho – yatukumbusha sote tulikotoka – sura ya pili ya Kitabu cha Mwanzo
– kuwa tuliumbwa toka mavumbi. Pamoja na tofauti zinazoweza kuwepo kati yetu n.k –
siku ya majivu tunakumbushwa kuwa wewe ni udongo na udongoni utarudi. Katika tendo
kama hilo – majivu huwa sasa mwaliko wa toba, kumrudia Mungu na kupokea maisha mapya.
Mwaliko wa Isaya – toeni tena si majivu bali mafuta.
Kwaresima yatuita tuingie
katika hali ya jangwa. Jangwa ni mahali pa uzao wa watu wa Mungu wa Agano la Kale.
Wayahudi toka utumwani Misri wanaingia nchi ya ahadi kama taifa moja chini ya Mungu.
Ni jangwani walifanyika Taifa la Mungu kwa njia ya agano. Katika mahangaiko yao, walipomwasi
Mungu n.k – Manabii wanawakumbusha warudi jangwani ili kujikumbusha wao ni nani, vifungo
vyao, ahadi ile, wito wao na utume wao kama njia tena ya kuiamsha imani yao na kuimarisha
tena agano lao na Mungu. Manabii Eliya na Yohani Mbatizaji walikuwa watu wa jangwani:
waliishi jangwani, walikula vyakula vya jangwani na wakaishi maisha yasiyo na makuu
ya jangwani.
Katika Injili ya leo tunasoma – Mk. 1:12-13 – mara Roho akamtoa
aende nyikani. Akawako huko jangwani siku arobaini, hali akijaribiwa na shetani, naye
alikuwa pamoja na wanyama wa mwitu, na malaika walikuwa wakimhudumia.
Ni wapi
tena zaidi ya Jangwani ambapo twaweza kukutana na Roho Mtakatifu na pia shetani, wanyama
wa pori pia malaika? Jangwani Yesu anapata muda wa kutofautisha sauti ya Mungu anayopaswa
kufuata na ile ya shetani ambayo ni kishawishi. Ni sauti ngapi tuzisikiazo tangu tuamkapo
hadi tuingiapo kitandani usiku? Pia sauti zetu na miito yetu ya ndani?
Jangwa
ni sehemu kubwa ambayo hizi sauti zinabaki nyuma. Jangwani tunapata nafasi ya kujifahamu
nguvu zetu na udhaifu wetu, pia sauti ya Mungu. Jangwani Yesu alikutana na wanyama
wakali na malaika. Wanyama wakali na pia malaika wapo katika kila mmoja wetu. Katika
hali zetu tunashindwa kutambua wanyama wakali na hivyo tunabaki vipofu na kujisifia
hovyo au tunashindwa kutambua malaika ndani yetu na hivyo kukata tamaa. Maisha jangwani
yanatupa nafasi tena – kuangalia tulikotoka, tulipo na tuendapo. Kwaresima yatupa
nafasi ya kutengeneza jangwa na kuangalia maisha yetu. Uelewa huu hutusaidia kujua
ni kipi cha kusema ndiyo kwa Mungu na hapana kwa shetani.
Katika Somo la 1
– Mungu anafunga agano na Nuhu na watoto wake baada ya gharika. Kadiri ya mwandishi
anaelewa agano hili kwa mtu wa kwanza kuwa ni kilelezo cha agano – Mwa. 1:28-30.
Hili
Agano la kwanza liliharibiwa na dhambi ya mwanadamu. Akiangalia ubaya wa dhambi, Mungu
anasikitika kwa kumwumba mwanadamu, na moyo wake ukaumia – Mwa. 6,6. Gharika yaonekana
kama Mungu anaingilia kati huko kwa mwanadamu kumkana yeye. Zuri na jema zaidi ni
kuonekana kwa matumaini – Nuhu anapendelewa na Mungu – Mwa. 6,8. Hivyo zama inapita.
Nuhu na familia yake wanamngojea Bwana. Naye Bwana anafanya tena kitu. Anafanya tena
agano na hao watu. Ni kama Mungu anasema tena ya zamani yamepiat. Yaliyopitwa si ndwele
tugange yajayo. Tuanze upya na upinde wa mvua unakuwa alama yao.
Na katika
Agano hili – Mungu anafanya agano na kila kiumbe na hapa mwisho viumbe vyote vitafanywa
upya – Rum. 8:18-22. Ufahamu wa Agano hili kati yetu na viumbe vyote ni alama ya upya
wa agano hili.
Injili – Yesu yuko Jangwani kwa siku 40, mwanzo wa kwaresima.
Inahusisha pia kuonekana kwake Galilaya na mwanzo wa utume wake. Hii pia ni mwanzo
mpya. Kwamba Yesu – uwepo wake ni mwanzo mpya unakubalika na wote wenye imani katika
maandiko matakatifu na kumkubali kama Mwana wa Mungu.Tungesoma sehemu iliyotangulia
tungesikia habari juu ya ubatizo wa Yesu. Mungu anatangaza rasmi kuwa Yesu ni mwanaye
mpendwa tumsikilize yeye. Huyu Mungu-mtu – sasa anawatembelea watu wake.
Pia
katika Injili – Roho Mtakatifu alishuka juu yake Yesu kama hua. Katika kuandika huku
kwake Yesu kukaa na wanyama pori –analinganisha maelezo ya Isa. 11,6 –mbwa mwitu atakaa
na mwanakondoo, na chui atakaa na mtoto. Kama ilivyo katika Nuhu, yote yaonekana kuanza
upya. Pamoja na yote tunayoweza kufanya katika kipindi hiki cha kwaresima, la msingi
zaidi ni kule kuwa tayari kuanza upya. Jambo moja ni hakika – upendo wa Mungu uko
mlangoni ili kutuimarisha na kutupa heri.