2015-02-20 09:37:26

Mahubiri yawe mafupi lakini yenye mashiko!


Mahubiri ni sehemu muhimu sana katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, ni tafakari inayolenga kugusa sakafu ya mioyo ya waamini, kwa kutambua kwamba, Padre anamwalikisha Yesu Kristo Kuhani mkuu anayependa kuwagawia waja wake Neno na Mkate wa uzima wa milele. Ni wajibu wa Kasisi kuhakikisha kwamba, anajitahidi kuyatamadunisha mahubiri yake kadiri ya tamaduni, mazingira, mila na desturi njema.

Ni wajibu wa Mapadre kujifunza sanaa ya mahubiri, ili kuwasaidia kuwakilisha barabara ujumbe wa Neno la Mungu kwa adhira inayokusudiwa, kwa kuzingatia sheria na kanuni za Kanisa. Altareni ni mahali patakatifu panapostahili heshima, nidhamu na ibada, kwani hapa Mwenyezi Mungu anatukuzwa na mwanadamu anatakatifuzwa. Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na majaribio ya kutaka kuwakonga na kuwagusa waamini wakati wa mahubiri kwa kuweka nyimbo zinazowachangamsha waamini, yote haya ni mambo mema.

Lakini inapaswa kukumbuka kwamba, Yesu Kristo Mkombozi wa dunia ndiye Kiongozi mkuu wa Ibada anayependa kuwaokoa na kuwakomboa watu wake kwa njia ya maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Yesu Kristo aliyechomwa mkuki ubavuni humo yakatoka maji na damu ni alama za Sakramenti za Kanisa zinazopaswa kuadhimishwa kwa moyo wa ibada na unyenyekevu mkuu. Ni Mafumbo ambayo yanaihusisha Familia ya Mungu, kumbe, Jumapili inakuwa kweli ni Siku ya Mungu, Siku ya Kristo, Siku ya Kanisa, Siku ya Binadamu na Siku ambayo waamini wanatafakari kuhusu Mambo ya Nyakati. Mahubiri yaguse undani wa mtu, ili kumsaidia kukua na kukomaa katika imani, matumaini na mapendo.

Hizi ndizo changamoto ambazo Baba Mtakatifu Francisko amependa kuwashirikisha Wakleri wa Jimbo kuu la Roma, alipokutana nao mjini Vatican siku ya Alhamisi, tarehe 19 Februari 2015. Mahubiri ni kati ya mambo ambayo Baba Mtakatifu Francisko anasema yanapaswa kupewa msukumo wa pekee kwa ajili ya kustawisha maisha ya kiroho ya waamini. Mahubiri yawe mazuri na mafupi kwa kuwahusisha waamini katika maisha yao ya kiroho, tayari kulimwilisha Neno la Mungu kama sehemu ya mchakato wa ushuhuda wa imani tendaji.

Waamini wafafanuliwe kwa ufasaha Mafumbo ya Kanisa na Wakleri wanaohubiri Neno la Mungu, wawe kweli ni mfano na rejea kwa Familia ya Mungu kwa kuyaweka hayo wanayohubiri katika matendo pamoja na kutambua kwamba, wao wamepakwa mafuta ili kuwatangazia Watu wa Mungu, Habari Njema ya Wokovu pamoja na kuwasaidia kuwaadhimishia Mafumbo ya Kanisa, ambayo ni haki yao msingi kama Wakristo. Mahubiri yarutubishwe kwa njia ya tafakari na sala, ili hatimaye, yaweze kumwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa.

Maneno na matendo ya Kiongozi wa Ibada yaoneshe kwa kina na mapana Mafumbo yanayoadhimishwa na Mama Kanisa pamoja na kutambua kwamba, Kiongozi mkuu wa Ibada ni Yesu Kristo! Padre awe ni shuhuda wa Mafumbo ya Kanisa mintarafu mwelekeo wa kichungaji. Fumbo la Ekaristi Takatifu liwawezeshe waamini kujisadaka na kujimega kwa ajili ya wengine, kwani hili ni tendo la upendo na haki.

Mahubiri ni sala ya Kanisa inayomwilishwa katika maisha ya watu, ni mawasiliano na ushuhuda wa maisha unaolenga kuwavuta waamini, ili kusali na kutafakari na Padre wakati wa mahubiri yake. Mapadre wajifunze kuhubiri vyema na kwa unyofu anasema Baba Mtakatifu Francisko. Padre awe makini kuchagua maneno ya kutumia katika mahubiri yake kwani si kila neno linaweza kufaa kwa ajili ya mahubiri. Padre ajiandae vyema kwa kufanya rejea kwenye nyaraka mbali mbali za Kanisa ili kuchota utajiri unaofumbatwa humo.

Padre anapoadhimisha Mafumbo ya Kanisa atambue uwepo wa Familia ya Mungu inayosali na kutafakari pamoja naye na kamwe asiwe ni "Msanii" Altareni; wala hakimu wa kutoa hukumu kwa waamini wake na wala Padre asiwe ni kiranja wakati wa mahubiri. Katika Ibada ya Misa Takatifu, Padre asiwe na kishawishi cha kutaka kuzungumza yote kwa wakati mmoja, aseme mahubiri machache yenye mvuto na mguso; mahubiri yanayoacha chapa katika sakafu ya mioyo ya Watu wa Familia ya Mungu.

Ni kutokana na changamoto kama hizi zilizotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati huo akiwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Buenos Aires kunako tarehe Mosi, Machi 2005 ndizo zilizofanyiwa kazi na Baraza la Kipapa la Ibada, Nidhamu na Sakramenti za Kanisa katika kuandaa Mwongozo wa mahubiri, uliozinduliwa hivi karibuni hapa mjini Vatican. Haya ndiyo ambayo yamekuwa ni msingi wa mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Wakleri wa Jimbo kuu la Roma, Alhamisi, tarehe 19 Februari 2015.







All the contents on this site are copyrighted ©.