Askofu mkuu Paulino Lukudu Loro, wa Jimbo kuu la Juba, Sudan ya Kusini, anawataka
viongozi wa kisiasa nchini humo kuhakikisha kwamba, wanajikita katika mchakato wa
ujenzi wa haki, amani na upatanisho wa kitaifa kama suluhu ya kuhitimisha vita ya
wenyewe kwa wenyewe iliyolipuka tena nchini humo zaidi ya mwaka mmoja uliopita. Ikiwa
kama vita hii haitaweza kusitishwa haraka iwezekanavyo, taifa la Sudan ya Kusini linaweza
kuangamia.
Askofu mkuu Paolino Lukudu Loro anawataka wananchi wote kutoka Sudan
ya Kusini, kujielekeza zaidi na zaidi katika kujenga na kudumisha umoja na mshikamano
wa kitaifa kwa kuondokana na ukabila ambao kwa sasa umepitwa na wakati, kwani hiki
kimekuwa ni kikwazo cha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Inasikitisha kuona
kwamba, maombi yanayotolewa na viongozi wa kidini ili kusitisha vita na kinzani za
kijamii mara nyingi yanagonga mwamba, lakini ikumbukwe kwamba, waathirika wakubwa
ni wananchi wa kawaida kwani viongozi wa kisiasa wataendelea kupata posho za vikao
na kuishi vizuri, huku wananchi wakiendelea kuteseka. Wananchi watambue kwamba, vita
bado inapamba moto huko Sudan ya Kusini.
Wakati huo huo, Askofu Edward Hiiboro
Kusala wa Jimbo Katoliki Tombura-Yambiro, Sudan ya Kusini anasema, uamuzi wa Serikali
wa kuahirisha zoezi la uchaguzi mkuu uliokuwa unapaswa kufanyika mwezi Juni mwaka
huu ni wa kishujaa na unapaswa kupongezwa na wapenda amani na maendeleo.
Hivi
karibuni, Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan ya Kusini katika mkutano wao uliofanyika
hivi karibuni walikuwa wameonya kwamba, kusingekuwepo na mafanikio makubwa katika
mchakato wa uchaguzi kama ungefanyika mwezi Juni. Kwa sasa, sensa ya watu na makazi
inaweza kuendelea na kuwa wabunge wataendelea kumalizia mchakato wa Marekebisho ya
Katiba ya Nchi, ili kujipanga vyema kukabiliana na changamoto za kipindi cha mpito.
Ikiwa kama mambo yote haya yatatekelezwa kikamilifu, basi hapana shaka kwamba,
uchaguzi mkuu unaweza kufanyika katika mazingira ya haki, amani na utulivu. Maaskofu
Katoliki Sudan ya Kusini wanawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali
na kuendeleza amani na utulivu nchini mwao.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.