Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amesema Serikali imepanga kuajiri walimu zaidi
ya 35,000 kwa ajili ya shule za sekondari ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa walimu
nchini. Ametoa kauli hiyo Alhamisi, Februari 19, 2015, wakati akizungumza na mamia
ya wakazi wa kata ya Kiwere, mara baada ya kukagua ujenzi wa maabara na kuzindua nyumba
nne za walimu kwenye shule ya sekondari ya Kiwere, tarafa ya Kalenga, wilayani Iringa.
Waziri
Mkuu alisema walimu hao watagawanywa kwenye shule kulingana na mahitaji yaliyokwishawasilishwa
na kwamba watakapopata mgao wao hawana budi kuziangalia kwanza shule zenye miundombinu
iliyokamilika kama ilivyo kwa shule hiyo. Akifafanua kuhusu kasi ya ujenzi wa maabara
Waziri Mkuu alisema: “Mkoa mzima wa Iringa unahitaji kuwa na maabara 318 na zilizo
tayari mpaka sasa ni 108. Lakini kuna nyingine 141 ambazo zimekwishaanza kujengwa
na zimefikia hatua nzuri. Nimeambiwa katika muda mfupi ujao kutakuwa na maabara 249
zilizokamilika,” alisema.
“RC inabidi uwasukume watu wako ili hizi 69 ambazo
bado hazijaanza kujengwa zikamilike kabla ya Juni mwaka huu kama ambavyo Mheshimiwa
Rais Jakaya Kikwete alikuwa ameelekeza. Alisema hataongeza tena muda wa ujenzi,” aliongeza.
Alisema elimu ni sekta ya msingi ambayo Serikali imeamua kuipa umuhimu wa kipekee
na kuiweka katika moja ya maeneo sita muhimu ya kipaumbele chini ya Mpango wa Matokeo
Makubwa ya Haraka (BRN).
Waziri Mkuu aliwataka wanafunzi wa shule hiyo
wasome kwa bidii na wawe wasikivu ili waweze kufanya vizuri zaidi kwenye masomo yao.
Mapema, akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Afisa Elimu wa Wilaya ya Iringa, Bw.
Leonard Msigwa alisema ujenzi wa nyumba hizo nne ambazo zina pande mbili (four duplex
houses) umegharimu sh. milioni 323.2. Alisema nyumba hizo zenye vyumba vitatu vya
kulala, sebule na jiko, zina uwezo wa kubeba familia nane.
Bw. Msigwa alisema
ujenzi wa nyumba ulifanywa shirika la DESWOS la Ujerumani kwa kushirikiana na Halmashauri
ya Wilaya ya Iringa pamoja na wananchi. Pia walisaidiwa kujengewa tanki la maji na
mabweni mawili yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 112 kila moja kwa ajili ya wasichana.
Akifafanua kuhusu hali ya ujenzi wa maabara, Afisa Elimu huyo alisema hadi sasa wamekamilisha
ujenzi wa vyumba viwili vya Kemia na Baiolojia lakini bado viko kwenye hatua ya kupaka
rangi. Alisema mfumo wa gesi na maji umekwishafungwa ndani ya vyumba vya maabara.
“Ujenzi
wa maabara hadi sasa umekwishagharimu sh. milioni 52.8/- na katika kipindi cha Februari
2015, tumefanikiwa kutengeneza baadhi yasamani za maabara yaani meza 24 na stuli 96
zenye thamani ya sh. 8,940,000/-,” alisema.