2015-02-19 09:16:58

Yatakatifuzeni malimwengu kwa njia ya ushuhuda!


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil kwa ajili ya Kampeni ya Udugu inayofanyika kila mwaka wakati wa Kipindi cha Kwaresima na kwa mwaka huu inaongozwa na kauli mbiu “Kanisa na Jamii” anawakumbusha kwamba, Kwaresima ni kipindi cha maandalizi ya Maadhimisho ya Fumbo la Pasaka. RealAudioMP3
Ni kipindi kwa toba, sala na matendo ya huruma, changamoto ya kufanya mageuzi katika maisha ya kiroho, kwa kujifananisha na Kristo kwa kujisadaka kwa moyo wa ukarimu na mapendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu anaikumbusha Familia ya Mungu nchini Brazil kwamba, Yesu alikuja duniani si kwa ajili ya kutumikiwa bali kutumikia na kutoa maisha yake ili yaweze kuwa ni fidia ya wengi.
Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika Waraka wao kuhusu Fumbo la Kanisa wanasema kwamba, watu wote wanaitwa katika umoja na Kristo aliye nuru ya ulimwengu, chanzo cha wokovu na kiini cha umoja, changamoto ya kusaidiana na kuhudumiana kwani Mama Kanisa anatambua kwamba, uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati zetu, hasa ya maskini, ya watu wanaoteswa yote ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia.
Siku arobaini za Kwaresima ni muda wa wongofu wa ndani na kampeni ya udugu nchini Brazil inalenga kuwasaidia kuona matukio mbali mbali katika maisha kwa mwanga wa Injili, ili kukuza na kudumisha majadiliano na ushirikiano kati ya Kanisa na Jamii kadiri ya maelekezo yaliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kama sehemu ya mchakato wa kukuza na kujenga Ufalme wa Mungu katika sakafu ya mioyo na maisha ya wananchi wa Brazil.
Baba Mtakatifu Francisko anakumbusha kwamba, Kanisa na Serikali ni taasisi mbili zinazojipambanua kwa huduma zake, lakini zinashirikiana kwa pamoja ili kulinda, kudumisha utu, heshima na mafao ya wengi ndani ya jamii. Kila mt una taasisi inapaswa kutekeleza dhamana na utume wake barabara sanjari na kuwasaidia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.
Kila mwamini anahamasishwa na Mama Kanisa kuwa ni chombo cha ukombozi na chachu ya maendeleo kwa maskini, ili hata nao waweze kushirikishwa kikamilifu katika shughuli za kijamii, daima waamini wawe makini kusikiliza kilio cha maskini na hatimaye, kuwasaidia kwa hali na mali.
Maskini waonjeshwe ukarimu, wapatiwe mahitaji yao msingi, wamegewe muda kama kielelezo cha sadaka na majitoleo ya watu, kwani kwa njia hii, hata wale wanaodhani kwamba, ni wafadhili, wanatajirishwa kutokana na huduma kwa maskini, kwa kujenga dhamiri nyofu, ili kuwasaidia wananchi kuwa kweli ni wajenzi wa jamii ambayo inasimikwa katika: haki, udugu na amani.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Yesu anapohubiri kwamba, amekuja ili kutoa huduma, anawachangamotisha wafuasi wake kupenda na kuhudumia. Kipindi cha Kwaresima iwe ni fursa kwa waamini kujisadaka kwa njia ya huduma na maisha mapya yanayopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo na kumwilishwa katika medani mbali mbali za maisha, ili kukuza udugu na ushirikiano.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.