Mzalendo ni mzawa anayependa pahala au nchi yake na yuko tayari kutetea hata kufa.
Mwananchi mvunjanchi huyo ni msaliti. Usemi wa zamani wa “mvunjanchi ni mwananchi”
unamhusu mzawa asiyekuwa na uzalendo kwa nchi yake. Usemi wa kisasa “Uzalendo umenishinda”
unatumika sana na waswahili wanaposhindwa kuutetea uzalendo wao, yaani kuishi itakiwavyo,
au hasahasa kutetea ukweli.
Tungeweza kusema pale mtu anaposhindwa kuishi kadiri
ya utu wa maisha yake. Mathalani mtu wa ndoa anapovunja uaminifu kwa ndoa yake anajituliza
“uzalendo umenishinda”. Maana yake ameshindwa kutetea maadili ya utu wa wito wake
au uzalendo kwa ndoa yake. Zamani mtu wa namna hii alijitetea na kusema: “Shetani
amenidanganya”. Shetani maana yake mpinzani, mhaini, msaliti, mdanganyifu, mwasi.
Kutokana na maana hizi shetani anaonekana kwa macho, kwa vile msaliti huyo, au mvunjanchi
na mkosa uzalendo ni wewe mwenyewe hasa pale unapokiri na kusema “Uzalendo umenishinda”.
Ndugu
zangu katika biblia kuna nyakati nyingi sana shetani anapoonekana kuwa mhaini, msaliti,
mshtaki, mdanganyifu, mwasi na kuwavunjisha watu uzalendo katika maisha yao. Kwa mfano
tukimwacha yule shetani aliyemdanganya Eva, yuko shetani yule aliyemsaliti au kumchongea
Ayubu kwa Mungu. “Ilikuwa siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha
mbele za Bwana, Shetani naye akaenda kati yao. Alipoulizwa na Mungu ametoka wapi,
akajibu “Natoka katika kuzungukazunguka duniani na katika kutembea huku na huku.
Kisha
Bwana akamwuliza shetani, “Je, umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu ni mtu mkamilifu….
Ndipo shetani akamjibu Bwana, na kusema, “Je, huyo Ayubu yuamcha Bwana bure?...Nyosha
mkono wako sasa uyaguse hayo yote aliyo nayo, naye atakukufuru mbele za uso wako.”
(Ayubu 1:6-11). Yaonekana shetani alikuwa na fursa ya kwenda kwa Mungu akijichanganyachanganya
na wenye haki, na huko akawa anatuchongea au kutushtaki kwa Mungu.
Yesu alipokuwa
hapa duniani “uzalendo haukumshinda” bali yeye alidumu kuwa mwaminifu kwa Baba yake,
licha ya kwamba alizingirwa na mashetani au wasaliti wengi waliotaka kumpotosha asiwe
mwaminifu kwa uzalendo aliotumwa kuuishi hapa duniani.
Kwa bahati nzuri wachongezi
na wasaliti hao yaani shetani hawana nafasi tena. Shetani ametupwa, hayuko tena mbinguni.
Hawezi tena kujichanganya na wengine kwenda kutushtaki kwa Mungu. Nyoka wa agano la
kale, yule aliyekuwa anatushtaki asubuhi na jioni kwa Mungu amefukuzwa mbinguni. Yesu
alisema, niliona shetani akishuka toka mbinguni kama radi, pale waliporudi wafuasi
wale sabini kwa furaha wakisema “Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako, Yesu akawaambia
‘Nilimwona Shetani akianguka kutokana mbinguni kama umeme’ (Lk. 10:17-18).
Sasa
mashetani tunayo hapahapa duniani. Wayahudi waliwaita wapinzani wao Wapersia kuwa
ni mashetani. Tunaona katika Injili Yesu anamwita Petro kuwa shetani, “Nenda nyuma
yangu, shetani, maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu” (Mk. 8:33). Watu
walio na fikra za kibinadamu na siyo za Mungu wanaitwa mashetani. Kadhalika watu wanaotaka
kuendeleza ufalme wao wa ukandamizaji, wa kudhulumu wengine hao ni ushetani.
Wainjili
Mateo na Luka wanasimulia kirefu na kwa mapana jinsi shetani alivyotaka kumsaliti
Yesu kwa kumpa vishawishi vitatu kule jangwani. Mosi kugeuza mawe kuwa mikate, pili
kumsujudia shetani ili kupata ufahari, tatu kujitupa toka mnara wa hekalu ili kudakwa
na malaika. Mwaka huu tunapata masimulizi ya vishawishi hivyo toka Injili ya Marko
katika aya mbili tu. Yatubidi tuzitafakari aya hizo kwa kina sana ili kuweza kupata
ujumbe kwa maisha yetu, kwani “Mwenzako akinyolewa wewe tia maji.”
Tunaambiwa:
“Mara Roho akamtoa aende nyikani. Akawako huko jangwani siku arobaini, hali akijaribiwa
na shetani;” Inashangaza sana kumwona Roho wa Mungu anamsukumia Yesu jangwani ili
akashawishiwe, kwa sababu katika sala aliyotufundisha Yesu mwenyewe, tunamwomba Mungu
Baba yetu “Usitutie katika kishwawishi.” Hapa yaonekana wazi kwamba Yesu hakupendelewa
kwa namna ya pekee, katika maisha haya bali alipitia vishawishi na matatizo kama binadamu
wengine nguvu za shetani zilitafuta kumpotosha kutoka uzalendo na maisha ya utu.
Ndiyo
maana neno la kigiriki peirazomenos maana yake kuwekwa kiti moto au
kujaribiwa. Wayahudi walikaa jangwani miaka jangwani siku arobaini walipotoka huko
wakawa washindi. Kwa hiyo jangwani ni mazingira yanayompa mtu fursa ya kukabiliana
na shetani ili aweze kuchukua maamuzi mazito ya kuishi uzalendo au kukubali kwamba
“uzalendo umemshinda.”
Namba hiyo arobaini ni fumbo na inamainisha maisha
yote ya binadamu. Maisha hayo yaweza hata kuwa siku chache tu za kuishi, kama ilivyo
usemi wa kiswahili “siku za mwizi ni arobaini”, haimaanishi mwizi anakamatwa zifikapo
siku hizo kwani mwizi mwingine hashikwi hadi uzeeni, lakini akikamatwa cha moto atakiona!
Kadhalika shetani, ni kitu chochote kile kinachotufanya tuwe mbali na Mungu, kwa hiyo
budi tukifahamu sawasawa jinsi kilivyo, kwa sababu kinachukua umbo la mwili, hivi
tunaweza kupambana nacho uso kwa uso.
Tunaambiwa tena kuwa kule jangwani Yesu,
“alikuwa pamoja na wanyama wa mwitu, na malaika walikuwa wanamhudumia.” Wanyama hao
siyo wale tunaowasikia katika kitabu cha Isaya kwamba katika ulimwengu ujao watu wataishi
kwa amani na wanyama, la hasha bali ni wanyama wale tunaowasikia katika kitabu cha
Daniele, yaani wanyama wanaowakilisha watawala kafiri ambao simba aliyewakilisha wafalme
wa Babiloni, dubu aliyewakilisha Wamedi na chui aliwakilisha Wapersia.
Watawala
wenye mamlaka wa ulimwengu huu na washawishi wa mambo ya kisiasa. Wakati wa Yesu wanyama
hao walilinganishwa na walimu wakuu, Makuhani, Wafarisayo, Masadukao wenye mamlaka
ya uchumi, Waandishi wanaohubiri vyema lakini wanashambulia nyumba za wajane na makuhani
wanamhubiri Mungu vizuri lakini hawakuyaishi maadili mema ya haki na upendo. Yesu
ilimbidi apambane hasa na wanyama kama hawa. Tujihadhari sana tusiwe sisi hao wanyama
wakali.
Hatimaye, tunawakuta “malaika walikuwa wakimhudumia”, Hapa malaika
haina maana ya kiroho, bali kila mwakilishi aliye chombo cha utumishi wa Mungu kwa
ajili ya kuhudumia binadamu. Tunaposema “wewe ni malaika”, hata Musa aliitwa Malaika,
kadhalika Yohane Mbatizaji aliitwa pia malaika. Yaani watu wale wanaojituma kumwakilisha
Mungu na kufanya matendo mema na mazuri kwa binadamu wenzao kwa jina lake.
Mathalani
malaika wa kwanza wa Yesu walikuwa ni Maria na Yosefu, halafu wakafuata watu wengine
waliomtumikia na kumwenzi kufanya kazi ya Mungu. Leo kuna malaika wengi wakristu,
wanaomtangaza Kristu hasa wanaoituliza mioyo ya waliopondeka na kuwahurumia wengine.
Ndugu
zangu, maisha yetu hapa duniani ni kama miaka arobaini, na kuna wanyama na malaika.
Tusikubali kuwa wanyama na kusema “uzalendo umenishinda” bali tuwe malaika wema wa
kuhubiri Injili ya haki, amani na upendo. “Baada ya Yohana kutiwa gerezani, Yesu akaenda
Galilaya, akiihubiri Habari njema ya Mungu akisema wakati umetimia na ufalme wa Mungu
umekaribia. Tubuni na kuiamini Injili” (Mk. 1:14-15). Huu ndiyo mwaliko kwetu wakati
huu wa Kwaresima.