2015-02-19 09:46:02

Tanzania na Malawi boresheni mahusiano!


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, Jumatano, Februari 18, 2015, amepokea Hati za Utambulisho za mabalozi wanne wapya ambao wataziwakilisha nchi zao katika Tanzania. Katika shughuli iliyofanyika Ikulu, Dar Es Salaam, Rais Kikwete amepokea Hati za Utambulisho za Balozi Hawa Olga Ndilowe wa Jamhuri ya Malawi, Balozi Jasem Ibrahim Al -Najem wa Dola ya Kuwait, Balozi Thamsanqa Dennis Mseleku wa Jamhuri ya Afrika Kusini na Balozi Chirau Ali Mwakwere wa Jamhuri ya Kenya.

Katika mazungumzo mafupi na Balozi Ndilowe baada ya kuwa amepokea Hati za Utambulisho wake, Rais Kikwete amesema Tanzania na Malawi ni nchi jirani ambazo zimekuwa na uhusiano mzuri na wa kihistoria. Rais Kikwete amesema kuwa sababu ya ujirani huo, Tanzania na Malawi zina wajibu mkubwa wa kutafuta namna ya kuboresha uhusiano wao kama ambavyo imekuwa miaka yote.

“Hatuna namna yoyote ya kutokuishi pamoja. Huwezi kuihamishia nchi katika sehemu nyingine duniani. Hivyo ni muhimu kwa nchi zote mbili kutafuta namna ya kumaliza changamoto zao kwa pamoja na kwa mazungumzo”. Rais Kikwete amemwambia Balozi Ndilowe.

Katika mazungumzo yake na Balozi Najem ambaye anakuwa balozi wa kwanza wa Dola la Kuwait nchini Tanzania baada ya nchi hiyo ya Kiarabu kufungua ubalozi wake, Rais Kikwete ameishukuru Kuwait kwa misaada ya maendeleo ambayo nchi hiyo imekuwa inaipatia Tanzania. “Kuwait ni nchi rafiki wa karibu wa Tanzania, na pia ni nchi ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo yetu kupitia mifuko mbali mbali ya maendeleo. Tunawashukuru sana.”

Rais Kikwete katika mazungumzo yake na Balozi Mseleku amemwambia balozi huyo kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini haujapata kuwa bora na mzuri zaidi kuliko sasa. “Hatuna tatizo lolote wala changamoto yoyote katika uhusiano kati ya nchi zetu mbili. Tunashirikiana na kuungana mkono katika ngazi zote kuanzia ngazi ya kanda, ngazi ya Bara la Afrika na ngazi ya kimataifa.”

Naye Balozi Mwakwere amemwabia Rais Kikwete kuwa ni heshima kubwa sana kwake kuwa Balozi wa Kenya katika Tanzania, nchi yenye sifa nyingi. “Kwangu mimi nasikia niko nyumbani kwa sababu kwetu ni pale Mombasa.” Ameongeza Balozi Mwakwere: “Kwa sababu ya umuhimu wa Tanzania kwetu Kenya, nchi yangu imeleta maofisa wawili wenye hadhi ya Balozi kwenye ubalozi wetu ambayo siyo kawaida katika nyanja za kidiplomasia.”








All the contents on this site are copyrighted ©.