Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya kwanza ya Kwaresima
Mpendwa mwana wa Mungu, ninakusalimu nikisema tumsifu Yesu Kristo. Ninatumaini uko
tayari kupokea ujumbe wa Neno la Mungu kwa furaha. Tuko tayari katika kipindi cha
kwaresima kipindi cha toba ambapo Mama Kanisa anatualika kujiweka tayari kwa njia
ya toba kuenenda tena katika uzima mpya tulioupokea wakati wa ubatizo.
Kipindi cha
Kwaresima, ni kipindi ambacho chatuweka tayari kwa Fumbo la Pasaka. Ni kipindi cha
mapinduzi ya kiroho, mapinduzi ya ndani, yaani kumtafuta Mungu zaidi kwa kuyatimiza
mapenzi yake. Mazoezi yote ya kiroho, kujinyima raha za kidunia, kufunga chakula ni
namna ya kuunganika na Kristu mteswa hadi ufufuko wake.
Ni kwa lengo la kubadili
maisha yetu ya ndani, Neno la Mungu Dominika ya kwanza latuambia kuwa Mungu anaanzisha
hali mpya ya maisha, yaani utu mpya, toka mafuriko tokeo la dhambi kuelekea maisha
mapya.
Katika somo la kwanza tunapata kusikia habari juu ya mafuriko ya Noa.
Kwa hakika jambo hili linatisha sana na laweza kuonesha na kutufikirisha kuwa Mungu
hatupendi na hivi anapenda angamizo hilo. Badala yake Mungu ni mwema daima! Jambo
la mafuriko ni tokeo la kiburi chetu na dhambi zetu sisi wenyewe. Kumbe, Mungu anaingilia
kati na anaanzisha utu mpya, familia mpya na anahaidi baraka na mambo mapya na kamwe
hakutakuwa na angamizo jingine kama hilo. Hili ndilo agano ambalo Mungu anafanya na
watu. (Mw. 9: 9-11) Upendo wake unaojionesha katika agano hauna masharti bali ni huruma
kamilifu itokayo katika mtima wake ambayo yaleta maisha mapya na mabadiliko mioyoni
mwa watu.
Mtume Petro katika barua yake ya I sura ya III anapowaandikia watu
wote anatupeni habari njema iletwayo na Yesu Kristu Mwana wa Mungu. Anasema kwa njia
ya Yesu ambaye hakuwa na dhambi, wote waliokuwa na dhambi yaani wasiokuwa haki wameweza
kuokoka. Ni kwa njia ya mauti ya msalaba sote tumekombolewa. Amevunjilia mbali kiburi
ambacho kilileta mafuriko katika Agano la kale, ameleta maisha mapya kwa mwanadamu.
Kristu ndiyo huruma ya Mungu, ndiye limbuko la wote waliokuwa wamezama katika dhambi.
Kama ambavyo Kristo ameenda zake mbinguni nasi kwa njia yake tukiitikia utume wake
hapa duniani tutaingia mbinguni.
Sehemu ya Injili ya Marko 1:12-15 inaanzisha
safari nzima ya Kwaresima, inakualika kutubu yaani kuungama dhambi zako mbele ya Mungu
ili uweze kupokea ujumbe wa Neno lake daima. Kwa njia ya toba tunaweza kupata nafasi
ya kuamini na kusadiki kina mafundisho yote ya Yesu Kristo mteswa na mchungaji mwema.
Toba ni mlango wa neema na imani yetu ni mlango wa umisionari. Wajibu huu ni mgumu
lakini Kristu mwenyewe ametupa mfano kamili, amejaribiwa na ameonja ugumu katika safari
yake ya kuokoa ulimwengu.
Bwana yuko jangwani kwa siku 40 akisali na kutafakari
kuhusu mapenzi ya Mungu. Katika jangwa anajaribiwa lakini anasonga mbele bila kuogopa
wala kukata tamaa. Jambo hili latufundisha kuwa, tunapoanza safari ya wokovu kwa njia
ya ubatizo tunapata Roho wa Mungu wa kutusaidia katika safari, hata hivyo hatukingiwi
majaribu bali tunaalikwa kukabiliana nayo kwa unyenyekevu jangwani tukitafakari kwa
furaha mapendo ya Mungu.
Yesu hakukaa jangwani kwa siku moja bali siku 40
zikimaanisha maisha yake mazima, ndiyo kusema nasi twapaswa kusali na kuomba maisha
yetu yote. Jangwa ni alama ya nguvu pinzani na hivi tunapobatizwa imani haiwi jambo
la lelemama bali ni shughuli pevu ambayo tunapaswa kuitenda siku kwa siku sasa na
mpaka mwisho wa maisha yetu hapa duniani.
Mpendwa mwana wa Mungu, ninakutakieni
kwaresima njema na maisha ya toba daima, ili kwa njia hiyo uweze kupokea imani na
msamaha wa dhambi na kwa namna hiyo kukaa tayari kupokea mavuno mwishoni mwa Kwaresima
lakini hasa uzima wa milele.
Toka Radio Vatican mimi ni Pd Richard Tiganya,
C.PP.S.