2015-02-19 10:31:57

Mbegu ya upendo, isaidie kutokomeza baa la njaa!


Baraza la Maaskofu Katoliki Canada katika Kipindi hiki cha Kwaresima linaendesha Kampeni dhidi ya baa la njaa na utapiamlo ambalo limekuwa ni chanzo kikuu cha maafa kwa watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, licha ya uzalishaji na uwepo mkubwa wa chakula duniani, hapa tatizo ni uchoyo na ubinafsi unaojikita katika utamaduni wa watu kutoguswa na shida pamoja na mahangaiko ya watu wengine duniani. Utu na heshima ya mtu imewekwa rehani na badala yake, fedha, mali na faida kubwa vimepewa kipaumbele cha pekee.

Kampeni ya Baraza la Maaskofu Katoliki Canada dhidi ya baa la njaa na utapiamlo wa kutisha duniani, inasimamiwa na Tume ya Maendeleo na Haki ya Baraza la Maaskofu Katoliki Canada kwa kuungana na Kampeni iliyozinduliwa kunako mwaka 2013 na Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationali kwa kuongozwa na kauli mbiu "familia moja ya binadamu, chakula kwa wote".

Hapa Maaskofu wanawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanaonesha ushuhuda wa imani katika matendo, kwa kujali na kuguswa na mahangaiko ya watu wanaoteseka kwa baa la njaa duniani. Lengo ni kuwajengea uwezo waamini kujisadaka, ili kugawana matunda ya kazi ya mikono yao na wasiokuwa na kitu, yaani "akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi".

Baraza la Maaskofu katika ujumbe wake wa Kwaresima kwa mwaka huu linabainisha kwamba, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujifunga kibwebwe ili kupambana na mambo yale yanayosababisha umaskini wa hali na kipato kwa watu takribani billioni moja. Ikumbukwe kwamba, chanzo kikubwa cha umaskini ni ukosefu wa haki, mambo yanayochagia pia kutoweka kwa misingi ya amani na utulivu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linapenda kujielekeza zaidi na zaidi kwa kugharimia mchakato wa mapambano dhidi ya baa la njaa duniani katika nchi thelathini, ili kuleta maboresho ya maisha kwa wananchi. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kutambua kwamba, umaskini unapata chimbuko lake katika mazingira ambamo hakuna haki, kumbe, haya ni mambo yanayopaswa kuvaliwa njuga na waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, ili haki ipatikane, amani na utulivu vitawale.

Baraza la Maaskofu Katoliki Canada katika ujumbe wake wa Kwaresima, linawaalika waamini kupandikiza mbegu ya upendo na mshikamano na watu wanaoteseka kwa baa la njaa kwa kuwashirikisha mapendo na matumaini katika imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma. Kwaresima kiwe ni kipindi cha kufanya tafakari ya kina kuhusu mahusiano ya mtu binafsi na Muumba wake, bila kuwasahau jirani walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linawaalika waamini na atu wote wenye mapenzi mema kupandikiza mbegu ya mapendo kwa kuchangia kwa hali na mali katika kampeni ya Kwaresima kwa Mwaka 2015.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.