2015-02-19 11:05:59

Kwaresima 2015: Familia kwanza!


Kardinali John Tong, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Hong Kong, China anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema katika Kipindi hiki cha Kwaresima kutoa kipaumbele cha kwanza kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kuendelea kuenzi uwepo na mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Anasema, raha na starehe zisizokuwa na mashiko wala mvuto zimekuwa ni chanzo kikubwa cha majanga katika maisha ya mwanadamu.

Watu wamemsahau Mwenyezi Mungu na kudhani kwamba, wao ndio waumbaji wanaopaswa kuheshimiwa na kuabudiwa, kiasi cha kusahau kuwa wao ni mavumbi na mavumbini watarudi na kwamba, kifo kitakua mchungaji wao daima! Inashangaza kuona kwamba, watu wamekengeuka na kutopea katika dhambi kiasi hata cha kusahau tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Hiki ni kiburi na jeuri ya mwanadamu ambayo inamfanya kujikweza kama "Mlima Kilimanjaro" lakini atashushwa chini na kuwa kama "soli ya kiatu".

Mwanadamu amemezwa mno na malimwengu kiasi hata cha kuhatarisha usalama wa maisha na afya yake. Vijana wengi wanadhani ndiyo mtindo wa maisha kwa kutumia dawa haramu za kulevya, kwa kujihusisha na ngono; kwa kukosa heshima na nidhamu kwa wazee na watoto pamoja na kuendelea kujitumbukiza katika matendo yanayovunja haki na amani. Mambo yote haya anasema Kardinali John Tong ni matendo yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Maadhimisho ya Kipindi cha Kwaresima, iwe ni fursa ya kutambua, kuthamini na kuenzi tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; kwa kuunganisha familia, ili kweli ziweze kuwa ni mashuhuda wa Kanisa dogo la nyumbani, shule ya sala na utakatifu wa maisha. Waamini wanahimizwa na Mama Kanisa kuwa kweli ni watangazaji wa Injili ya Familia kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia katika jamii, kwani matumaini ya binadamu kwa siku za usoni, yanajikita katika maisha ya ndoa na familia.

Waamini wanachangamotishwa kusimama kidete, kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia na kamwe wasikubali kuyumbishwa kama gari bovu na sera pamoja na mikakati inayotaka kukumbatia utamaduni wa kifo pamoja na mahusiano tenge yanayotaka kuhalalisha ndoa za watu wa jinsia moja kama sehemu ya haki za binadamu. Waamini na watu wenye mapenzi mema wajitahidi kuishi maisha ya ndoa na familia kwa kushirikishana na kumegeana tone la upendo pamoja na kujitahidi kutumia muda wao ndani ya familia ili kuboresha mahusiano mema ndani ya familia.

Kardinali John Tong, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Hong Kong, China anawataka waamini kujisadaka katika kipindi hiki cha Kwaresima, ili kuwaonesha jirani zao mshikamano wa upendo na udugu unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Ni wakati wa kufanya maboresho ya mahusiano katika familia na jamii kwa ujumla wake; kwa kuombana toba na msamaha; kwa kumwilisha huruma na upendo katika safari ya maisha ya kila siku; kwa kutafuta suluhu ya kinzani na migogoro, ili kweli amani na utulivu viweze kutawala katika mioyo ya watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.