Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil katika kipindi cha Kwaresima mwaka huu sanjari
na maadhimisho ya siku ya 52 ya Kampeni ya udugu na mshikamano, limeamua kujikita
katika mambo makuu mawili yaani: Kanisa na Jamii kama sehemu ya kauli mbiu ya kipindi
cha Kwaresima, kinachowachangamotisha waamini kwa namna ya pekee kujenga na kudumisha
upendo na mshikamano wa kidugu. Waamini wanakumbushwa
kwamba, Yesu Kristo alikuja hapa duniani si kuhudumiwa, bali kuhudumia na kuyamimina
maisha yake ili yaweze kuwa ni fidia ya wengi. Jumatano ya Majivu, iwe ni siku ya
kuwakumbusha Wakristo, wito na utume wao na umuhimu wa Jumuiya za waamini kujenga
na kudumisha mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi na jamii inayowazunguka,
changamoto iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Waamini wanakumbushwa
kwamba, wako ulimwenguni kwa ajili ya kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda
wa maisha unaojikita katika haki, amani na maridhiano kati ya watu. Ni changamoto
ya kuhakikisha kwamba, wanazingatia utawala wa sheria, kwa ajili ya ustawi, maendeleo
na mafao ya wengi. Kipindi cha Kwaresima, wanasema Maaskofu Katoliki Brazil kwamba,
ni muda muafaka wa kujikumbusha kwa mara nyingine tena Nyaraka za Mababa wa Mtaguso
mkuu wa Pili wa Vatican; mafundisho yanayolitaka Kanisa kushiriki kikamilifu katika
maisha ya watu duniani: Liwe ni Kanisa linalofariji na kuonesha huruma kama ilivyokuwa
kwa yule Msamaria mwema. Wananchi wote wanaounda jamii ya Brazil, ni watoto wateule
wa Mungu. Kumbe, ni wajibu wa Wakristo kuhakikisha kwamba, kwa njia ya ushiriki
wao wanasaidia mchakato wa maboresho ya miundo mbinu, sheria na mashirika ya kijamii,
ili yaweze kuwa kweli ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu, ustawi na mafao ya wengi. Baraza
la Maaskofu Katoliki Brazil, katika ujumbe wake wa Kampeni ya upendo na udugu, linafafanua
kwa kina na mapana: historia ya uhusiano kati ya Kanisa na Jamii ya Brazil; hali ya
Brazil kwa sasa na changamoto zake. Maaskofu wanaangalia huduma ya upendo na mshikamano
inayotolewa na Kanisa Katoliki nchini Brazil; mwingiliano na tofauti kati ya Kanisa
na Jamii. Sehemu ya pili ya tafakari hii ambayo kimsingi ni mwongozo wa Baraza
la Maaskofu Katoliki Brazil, inafafanua mahusiano kati ya Kanisa na Jamii mintarafu
mwanga wa Neno la Mungu, Mafundisho ya Mababa wa Kanisa pamoja na Mafundisho Jamii
ya Kanisa. Sehemu ya tatu, Maaskofu wanaipembua jamii ya Brazil mintarafu huduma,
majadiliano na ushirikiano kati ya Kanisa na Jamii kwa kutoa kipaumbele cha kwanza
kwa utu, heshima, mafao ya wengi na haki jamii. Maaskofu wanatoa vielelezo makini
vinavyoweza kutumika kwa ajili ya kumwilisha ujumbe wa upendo na mshikamano wa kidugu
wakati wa Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka huu. Mwishoni, Baraza la Maaskofu Katoliki
Brazil, linaonesha mafanikio yaliyopatikana kwenye Kampeni ya mshikamano wa upendo
na udugu kwa mwaka 2014 pamoja na miradi iliyotekelezwa kama kielelezo cha ukweli
na uwazi katika matumizi ya fedha ya Kanisa inayolenga kuwahudumia maskini na wote
wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kunako Mwaka 2016, kutafanyika mshikamano
wa upendo na udugu wa kiekumene, kwa kutambua kwamba, kama Wakristo ni wamoja na huo
ni wajibu wao. Hii itakuwa ni mara ya nne kwa Baraza la Makanisa nchini Brazil kuandaa
kampeni ya kiekumene. Hii ni kampeni ambayo italishirikisha Shirika la Misaada
la Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani, “Misereor”, ambalo kwa miaka mingi limekuwa
mstari wa mbele katika kugharimia miradi ya maendeleo: Barani Afrika, Asia na Amerika
ya Kusini. Lengo ni kukuza na kudumisha mchakato wa maendeleo endelevu kwa ajili ya
kuboresha huduma ya afya na utu wa kila binadamu. Kwa mara ya kwanza kampeni hii iliendeshwa
kunako mwaka 2000, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Utu wa binadamu na amani”. Na Padre
Richard A. Mjigwa, C.PP.S Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.