Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi, Jumatano tarehe 18 Februari 2015 ameendelea
kujikita katika Familia, baada ya kupambanua kwa kina na mapana nafasi na dhamana
ya Mama, Baba na Watoto katika maisha na utume wa familia, Baba Mtakatifu ameendelea
kufafanua umuhimu wa kudumisha udugu katika familia, neno ambalo lina maana ya pekee
katika Ukristo sanjari na historia ya Ukombozi.
Baba Mtakatifu anasema, udugu
unaoundwa na kaka na dada katika familia ni uzoefu na mang'amuzi ya kibinadamu ambayo
kwa namna ya pekee yanapata mwangwi wake katika maisha ya Yesu Kristo aliyediriki
kuwaita ndugu zake, kwani wote ni watoto wa Mungu Baba Mwenyezi. Historia ya Kaini
na Abeli inadhihirisha kwamba, kila mtu anapaswa kuwa ni mlinzi na msimamizi wa ndugu
yake katika mfumo wa Familia ya binadamu.
Baba Mtakatifu anasema, ndani ya
Familia watu wanajifunza kuwa ni watu wema; na kwamba, kile ambacho mtu anajifunza
kutoka katika familia yake nyumbani kinakuwa ni chimbuko la utajiri mkubwa kwa jamii
katika ujumla wake. Neema ya Kristo inawawezesha waamini kuwaona watu wengine kuwa
ni Kaka na Dada, kwa kupatanisha tofauti na kinzani ili kujenga matumaini ya Jamii
inayosimikwa katika uhuru na usawa.
Upendo wa kidugu unajionesha kwa namna
ya pekee kabisa kwa njia ya huduma kwa watoto wenye matatizo maalum. Yesu anawafundisha
wafuasi wake kutambua kwamba, wanapaswa kuwaonesha watu wote upendo, lakini kwa kutoa
kipaumbele cha kwanza kwa wahitaji zaidi. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, jamii
zitaweza kujifunza kujenga na kudumisha moyo wa udugu na kwamba, familia sehemu mbali
mbali za dunia zitaweza kufurahia baraka kuu kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayojionesha
kwa vijana wanaopenda na kupendwa kama ndugu wamoja.
Mara baada ya Katekesi
yake, Baba Mtakatifu Francisko kwa mara nyingine tena, amewaomba waamini na mahujaji
waliokuwa wamefika mjini Roma kusikiliza Katekesi yake, kusali kwa ajili ya kuwaombea
ndugu zao Wakristo kutoka Misri, waliouwawa kikatili hivi karibuni nchini Libia kwa
vile tu, walikuwa ni Wakristo. Baba Mtakatifu anawaombea ili Mwenyezi Mungu aweze
kuwapokea katika makao yake ya milele pamoja na kuendelea kuwafariji ndugu na jamaa
walioguswa na msiba huu mzito.
Baba Mtakatifu pia anaendelea kuwataka waamini
kusali kwa ajili ya kuombea haki na amani huko Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini
kwa kuwakumbuka marehemu wote, waliojeruhiwa pamoja na wakimbizi. Ni matumaini ya
Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itaweza kupata suluhu ya amani
huko Libya, ambayo kwa sasa imegeuka kuwa ni uwanja wa fujo!
Baba Mtakatifu
Francisko akiwasalimia waamini na mahujaji kutoka Mashariki ya Kati amewaambia kwamba,
kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, uzoefu na mang'amuzi ya udugu katika maisha ya binadamu,
waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuwaonjesha
watu wote ukarimu, lakini zaidi kwa maskini na wahitaji zaidi.
Yesu ameanzisha
udugu unaovuka mipaka ya: rangi, lugha na tamaduni kwa kuwakumbatia wote, kiasi cha
kumwita Mwenyezi Mungu, Baba Yetu. Baba Mtakatifu anawataka waamini kukuza na kuimarisha
urafiki na mshikamano katika maisha na utume wa Kanisa: Parokiani na katika maeneo
ya kazi; maeneo muhimu sana katika kujenga na kudumisha udugu unaojikita katika upendo
wa Kiinjili, sadaka na mshikamano wa dhati.
Baba Mtakatifu ameombea pia amani
nchini Ukraini na kutambua uwepo wa Watawa wa Shirika la Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa
ajili ya Katekesi vijijini kutoka Zambia. Amewakumbuka pia wanashirika wa Uamsho wa
Kikristo kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaoungana kwa pamoja kwa ajili ya Ibada
ya Kuabudu Ekaridti Takatifu, anawahimiza vijana wa kizazi kipya kujitahidi kwenda
kukutana na Yesu. Kwaresima ni kipindi maalum anasema Baba Mtakatifu kwa ajili ya
kuimarisha maisha ya kiroho, kwa kufunga na kusali; kwa kutawala na kudhibiti vilema
katika maisha.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya
Radio Vatican.