2015-02-18 08:34:05

Toba!


Kipindi cha Kwaresima ni wakati muafaka wa kuhakikisha kwamba, fadhila za Kikristo zinamwilishwa kikamilifu katika maisha yanayojikita katika mapambano dhidi ya dhambi, ili kuwa kweli ni watakatifu kama Mwenyezi Mungu alivyo mtakatifu. RealAudioMP3
Ili kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano na Mwenyezi Mungu kuna haja ya kutubu na kumwongokea Mungu, kwa kuacha dhambi na nafasi zake, kwani dhambi si sehemu ya asili ya binadamu bali ni matokeo ya kiburi cha mwanadamu kama wanavyosema Mababa wa Kanisa. Waamini wanapaswa kuwa mbali na dhambi, kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji.
Utakatifu ni sifa kuu ya Mwenyezi Mungu ambayo anamshirikisha mwanadamu katika maadhimisho mbali mbali ya Mafumbo ya Maisha na utume wa Kanisa, lakini kwa namna ya pekee katika Adhimisho la Fumbo la Pasaka. Wakristo wanapopokea Mwili na Damu ya Kristo, wanapokea neema na baraka zinazowachangamotisha kuwa watakatifu pamoja na kujisadaka kwa ajili ya wengine; kwani wao pia wanakuwa ni sehemu ya Kristo ambaye ni Bwana na kielelezo cha utukufu wa Mungu. Waamini wanatakatifuzwa kwa kushiriki Mwili na Damu ya Kristo, changamoto ya kuendelea kuwa kweli ni watakatifu kwa kuwatakatifuza jirani zao kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji.
Hii ni sehemu ya ujumbe wa Kwaresima kwa Mwaka 2015 unaotolewa na Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli. Anasema, mwanadamu hana budi kupambana kufa na kupona dhidi ya dhambi na maelekeo yake, ili kurudisha tena ile adhi ya kwamba, ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, hii ni sehemu ya mchakato wa kazi ya ukombozi. Kwaresima ni kipindi maalum cha sala na tafakari, ili kuratibu maonjo na matamanio ya binadamu. Ni sehemu ya mchakato wa maandalizi ya Sherehe ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mungu na jirani ili kuweza kuungana na Watakatifu wa Mungu kumshangilia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu.
Mwanadamu katika hija ya maisha yake ya kila siku, anajikuta akitumbukia na kuogelea katika lindi la dhambi na mauti, kumbe kuna haja ya kukiri udhaifu wa kibinadamu na kunuia kutotenda tena dhambi, lakini pale mwamini anapoelemewa na udhaifu wa mwili, basi aoneshe pia ujasiri wa kukimbilia huruma na upendo wa Mungu, ili kurudisha tena ile neema ambayo waamini walijipatia wakati walipopokea Sakramenti ya Ubatizo.
Kwaresima ni kipindi cha kubadili mtindo wa maisha kwa kujikita katika fadhila ya upendo kwa Mungu na jirani kwa njiaya matendo ya huruma. Kwaresima ni kipindi cha kuwaonjesha wengine furaha na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake, kwa kujikita katika sala na tafakari ya Neno la Mungu; kwa njia ya usafi kamili pasi na mawaa! Waamini wajibidishe kufunga ili kuratibu vilema na mapungufu yao ya maisha.
Patriaki Bartolomeo wa kwanza katika ujumbe wake wa Kwaresima anabainisha kwamba, hiki ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani; fursa ya kusafisha dhamiri, ili ziweze kuwa nyeupe kama theluji, kwa kujikita katika fadhila ya upendo kama njia na kielelezo cha maisha na wokovu wa dunia. Kwa njia hii waamini wataweza kupata huruma na upendo wa Mungu kutoka kwa Kristo Mfufuka. Katika mapambano dhidi ya dhambi, waamini wanakumbushwa kwamba, wanaye Mama Bikira Maria pamoja na watakatifu walioko mbinguni, wanaoweza kuwasaidia kusafisha dhamiri ili kweli kuwa watakatifu mbele ya Mungu na binadamu.
Kwaresima iwe ni fursa ya kutafakari kwa kina na mapana fadhila za Kikristo; kufanya toba na wongofu wa ndani kwa kukimbilia huruma na upendo wa Mungu; ili kushiriki kikamilifu katika maisha mapya yanayobubujika kutoka kwa Kristo Mfufuka.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.