Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa hapo tarehe 19 Februari 2015, kukutana na kuzungumza
na Wakleri kutoka Jimbo kuu la Roma kuhusu umuhimu wa mahubiri katika maadhimisho
ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Baba
Mtakatifu atatoa tafakari na baadaye atawaalika Wakleri kuuliza maswali ili kuondoa
duku duku katika miyo yao anasema Kardinali Agostino Vallini, Makamu Askofu wa Jimbo
kuu la Roma katika barua aliyowaandikia Wakleri wa Jimbo kuu la Roma. Hii ni fursa kwa
Baba Mtakatifu kukutana na kuzungumza na Wakleri wa Jimbo kuu la Roma, walau mara
moja kwa mwaka, kadiri ratiba na shughuli za kichungaji zinavyoruhusu, kwani huu ni
muda muafaka wa furaha na matumaini mapya katika maisha na utume wa Kanisa. Mahubiri
katika Ibada ya Misa Takatifu ni kati ya mada ambazo Baba Mtakatifu anapenda kuzipatia
kipaumbele cha pekee, ili kuwaandaa waamini kuyafahamu Mafumbo ya Kanisa, tayari kujisadaka
na kuyatolea ushuhuda kama kielelezo cha imani tendaji, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza
kwa maskini. Mambo haya yanafafanuliwa vyema na Baba Mtakatifu mwenyewe katika Waraka
wake wa kichungaji, Injili ya Furaha. Kiongozi wa Ibada hana budi kuonesha moyo
wa ibada na unyenyekevu mkuu wakati wa kuadhimisha Mafumbo uya Kanisa, ili aweze kuwashirikisha
na kuwamegea waamini, kile ambacho ni matunda ya ukomavu wa imani inayorutubishwa
kwa Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa bila kusahau matendo ya huruma. Mahubiri
ni sanaa inayobubujika kutoka katika moyo wa sala na ibada, kwa kutambua kwamba, Kiongozi
wa Ibada anamwakilisha Yesu Kristo ambaye ndiye kiongozi mkuu anayependa kuwalisha
watu wake kwa Neno la Sakramenti. Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha Wakleri
kwamba, maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu si tendo la huruma bali ni haki
kwa Familia ya Mungu. Kumbe, mahubiri, si swala la kusoma, bali ni sanaa ya kutangaza
Neno la Mungu, linalotafakariwa katika hali ya sala na ukimya, ili kumwachia nafasi
Mwenyezi Mungu aweze kuzungumza na waja wake kutoka katika sakafu za mioyo yao. Kiongozi
wa Ibada atambue kwamba, Altare si mahali pa kufanyia mchezo wa kuigiza wala uwanja
wa kisiasa, bali ni mahali pa sala na sadaka inayopaswa kuadhimishwa kikamilifu ili
Mungu aweze kutukuzwa na mwanadamu atakatifuzwe. Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.