Tunaanza na Jumatano ya Majivu: siku 40 kabla ya siku tatu kuu zinazotangulia Pasaka,;
yaani mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo = KIINI CHA FUMBO LA WOKOVU
WETU. Katika kipindi hiki, wakristo wanaalikwa kutafakari sana fumbo la wokovu wa
Kristo na kuishi ubatizo wao kwa undani kabisa. Ni siku 40 za utakaso. Zaidi ya hayo,
twakumbuka siku 40 alizokaa Yesu jangwani – akisali na kufunga – kabla ya kuanza utume
wake hadharani.
Leo tunaungana na wakristo wenzetu kufuata njia ya msalaba,
ile ya Kalvari, tukitafakari kwa kina maana ya imani yetu na tukiishi katika matendo
kile tunachokiamini. Leo tunapakwa majivu. Maana yake nini? Katika kitabu cha Mwa.
3,19 tunasoma hivi; kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi,
ambayo katika hiyo ulitwaliwa, kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi.
Tutapakwa
majivu utosini au kisogoni. Maana yake nini? Alama hii yatukumbusha kuwa mwili wa
mwanadamu u katika hali ya uharibifu na ukomo – alama hii ikituelekeza kwenye matumaini
makuu. Tunaishi tukitambua kuwa sisi si kitu na ulimwengu huu ni mahali pa kupita
tu. Tunakiri na kukubali waziwazi mbele ya Mungu Baba Muumba wetu na mbele ya wenzetu
kuwa sisi tumepungukiwa. Ni majivu tu. Lakini huruma ya Mungu ni kubwa kuliko dhambi
zetu. Tunakiri dhambi zetu.
Mtu mmoja anafanya tafakari hii: majivu ni masalio
ya moto, makazi yake jalalani. Ila yakisugua sufuria yenye masizi huifanya kuwa nyeupe
pe. Japo tu dhaifu, tuna thamani zaidi ya majivu. Majivu yatufanye tuwe weupe.
Alama
ya pili ni sauti ya Yesu. Katika Mk. 1, 16 – tubuni na kuiamini Injili – mwanzo wa
safari ya kitume ya Yesu – mwaliko wa kuelekeza matumaini yetu katika Neno la Mungu.
Kipindi hiki kama tulivyosikia hapo juu – tunaalikwa kuwa karibu zaidi na Neno la
Mungu kwa imani na matendo. Maisha ya Mkristo ni maisha ya imani, yenye msingi wake
katika Neno la Mungu – na anayelishwa na Neno la Mungu anao uzima wa milele. Njia
kuu ya kushinda vishawishi na dhambi ni kusikiliza Neno la Mungu – ili kuwa na uwezo
wa kukataa vishawishi vya shetani.
MHIMILI WA KWARESIMA - kusikiliza Neno la
Mungu = neno la ukweli, kuishi, kusema na kutenda ukweli na kukataa uongo ambao ni
sumu kali inayoharibu ubinadamu wetu na mahusiano yetu na Mungu na wenzetu na ambao
pia ni mlango wa dhambi zote.
Kipindi cha kwaresima ni kipindi cha toba katika
Kanisa Katoliki cha siku zipatazo 40 tangu Jumatano ya majivu mpaka siku kabla ya
siku 3 kuu zinazotangulia Jumapili ya Pasaka au Jumapili ya ufufuko wa Bwana. Tunapofunga
tunahitaji kuzuia vilema vyetu na kuviacha kabisa, tunaomba kujaliwa moyo wa toba,
tunainua mioyo yetu na tunaomba Mungu atujalie nguvu na tuzo. Haitoshi tu kukiri makosa
yetu bali tunahimizwa kuungama na kutubu hayo makosa na kuwa tayari kuanza upya. Kipindi
cha kwaresima huanza tangu Jumatano ya majivu. Mwanzoni mwa kazi yake ya kuhubiri
Habari njema Yesu anaanza kwa kusema tubuni na kuiamini Injili – Mk 1,15. Maneno haya
haya tutayasikia/tumeyasikia tena leo tulipopakwa majivu. Mwaliko huu wa Yesu unatuingiza
katika kipindi cha toba – tubuni na kuiamini Injili. Huu ni mwaliko wa uzima. Ni mwaliko
ili tuongoke, tuanguke maisha mapya, maisha ya sala, kufunga na kutoa sadaka.
SALA. Kwa
kifupi kusali kwa Mkristo maana yake ni kuruhusu upendo wa Mungu utawale ndani ya
mioyo yetu na hivyo kuwa katika mwelekeo wa kusikiliza sauti za ndani ya mioyo ya
mwanadamu na kujiweka mbele yake na vyote tulivyo navyo. Kusali kwa mkristo ni kuishi
maisha ya sala kama sadaka na sifa kwa Mungu Muumba wetu. Sala pia inatuunganisha
na Yesu, kanisa na historia yake kwa ujumla na inatusaidia kufunua mioyo yetu mbele
ya Roho Mtakatifu ambaye anafanya kila kitu kuwa kipya, kwa ufupi sala katika utatu
Mtakatifu ndiyo jambo ambalo kila mwanadamu anapaswa kulitambua na kuligundua kipindi
hiki.
KUFUNGA. Kufunga kwa asili ya kiroho ina maana kubwa katika elimu
ya mambo ya mwisho hasa inapotokea kuwa kuna jambo kubwa linalosubiriwa. Ni kama vile
mahitaji ya mwanadamu ya kula yanashika nafasi ya pili kwa vile mwanadamu analishwa
na hamu hiyo na matarajio hayo. Hicho ndicho chakula chake.
Utamaduni wa kikristo
wa kufunga unawakilisha zaidi ya yote ukomo wa matarajio ya kumngoja bwana na kufungua
mioyo yao, na kujinyima kwa kilakitu ambacho kinaonekana kuwa ni kikwazo kuwa karibu
na Mungu. Ni kungojea kwa hamu kubwa, chukua mfano wa mtu anayeshinda njaa akipata
chakula atakavyokifurahia. Kwa kufunga tunatengeneza nguvu za kutawala miili yetu,
vionjo vyetu n.k. Kwa kufunga tunakuwa na uwezo wa kuiambia miili yetu kile tutakacho
kufanya.
Mfano tunajinyima chakula fulani kitamu, kizuru au kitu kitamu na
kuzuri tukipendacho na katika kujinyima huko tunatoa msaada au kujinyima huko tunawasaidia
wengine ili nao washiriki nasi upendo huo. Au kwa kutoendeleza mapenzi yetu tu, tukijinyima
kufanya hilo tulipendalo tunapata muda wa kufanya jambo fulani jema kwa ajili ya wengine.
Na hapa wakristo wanaalikwa kuwa makini – huwezi kufunga na kufaidi tena hicho hicho
unachopenda kukiacha. Kwa tendo la kufunga tunapata uwezo wa kuiambia miili yetu kile
tupendacho kufanya na si miili yetu ituambie kile cha kufanya.
Kwa maana hiyo
basi, kufunga kunamaanisha ni hija kuelekea kipindi cha pasaka na hivyo mwanadamu
anapaswa kutambuu kuwa tunamhitaji Mungu kama chanzo cha uwepo wetu na pia kujiweka
wazi ili Mungu aweze kuwa ndani yetu.
MATENDO YA HURUMA – KUTOA SADAKA Matoleo
mengineyo mema zaidi ya utoaji wa sadaka pia ni mwelekeo wa moyo. Moyo ambao ni mpole,
wa toba, wenye huruma na wa faraja ambao unatafuta mahusiano na wengine katika kuhurumia
wengine ili kukuza mahusiano na Mungu. Kwa hiyo au sadaka yaonesha kujali, kufanyakitu
halisi, zawadi ambayo waamini wanatoa wanapojaribu kuwazia upendo wa Mungu ambao unawakubali
na kuwasamehe. Je, Mungu ametujalia mambo mangapi mema? Sisi tumemrudishia nini? Kwa
asili na maana ya kutoa sadaka ni kupoteza pia. Huwezi kutoa sadaka na kutarajia hapo
hapo kufaidi yote pia. Mfano mzuri ni Bwana wetu Yesu Kristo – alitoa uhai wake kwa
ajili yetu. Hii ndiyo changamoto iliyo mbele yetu leo hii. Ni wangapi tuko tayari
kutoa sadaka kwa ajili ya wengine? Kujitoa kweli kwa hali na mali? Bila manung’uniko?
Bila kudai faida?
Hakika kipindi hiki cha kwaresima ni muda wa kuangalia upya
thamani ya sadaka ndogo, alama ya upendo, inayotolewa kwa unyenyekevu, kwa siri na
ambayo ni halali, ambayo inakugharimu, na inafanywa katika kumtukuza Mungu katika
wale wanaotaabika, na wahitaji. Tukijenga tabia au mazoea ya kutoa kwa ajili ya wahitaji
tunajenga pia mazoea ya kuwa huru na mambo ya dunia hii yanayopita. Kila mmoja wetu
ana hitaji fulani katika maisha yake, hakuna tajiri kabisa kwamba hana cha kupokea
au maskini sana kwamba hana cha kutoa. Kutoa ni moyo na si utajiri. Tuonje tena katika
kipindi hiki furaha ya kutoa kuliko ile ya kupokea.
Namalizia kwa kusema upendo
bila sadaka, hivyo hivyo upendo bila sadaka inakuwa kama alama ya nje tu. Sadaka ni
matoleo ya upendo na tusisahau mfano mkubwa alioutoa Bwana wetu Yesu Kristo ambapo
alisema Mungu alitupenda sana akamtwaa mwanae wa pekee kwa ajili yetu sisi sote. Kama
Mungu amejitoa kwetu je sisi tunamrudishia nini?
Kufunga kwaonesha heshima
yetu mbele ya Mungu, kutambua na kukubali udhaifu wetu mbele ya Mungu na wenzetu (kujipaka
majivu) kwamba tu wadhambi na kuwa tayari kufuata njia ya Bwana, yaani njia ya wokovu.
NASI TUINGIE KATIKA NJIA YA BWANA ILI TUWEZE KUPATA WOKOVU WA MUNGU.