2015-02-18 09:45:58

Jangwa la Sahel!


Wakurugenzi watendaji wa Mfuko wa Yohane Paulo II kwa ajili ya Sahel, hivi karibuni wamehitimisha mkutano wao wa mwaka, uliokuwa unaongozwa na Askofu mkuu Giovanni Pietro Dal Toso, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum, huko Dakar, Senegal. Anasema, kwa miaka mingi waamini wa dini mbali mbali Barani Afrika waliweza kuishi kwa amani na utulivu, huku majadiliano ya kidini yakijikita katika uhalisia wa maisha, kwani jamii ilijitahidi kuthamini dini, mila na desturi na masharti ya dini nyingine hata katika mambo ya kawaida kabisa!

Leo mambo yamechafuka kutokana na misimamo mikali ya kidini, hali ambayo inaendelea kusababisha mpasuko na migawanyiko ya kijamii kwa misingi ya kidini, kiasi kwamba, leo hii ni waamini wa dini mbali mbali wanaangaliana kwa mashaka na "macho ya makengeza". Hapa Mama Kanisa hana budi kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene, katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi katika Ukanda wa Sahara.

Mfuko wa Yohane Paulo II kwa ajili ya Sahel unatoa huduma na kuchangia maendeleo ya wananchi walioko kwenye Ukanda wa Sahel pasi na ubaguzi wa kidini au wa kikabila, kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Mfuko huu ni kielelezo makini cha ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo kadiri ya maelekezo ya Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ukanda wa Sahel unakabiliwa na changamoto nyingi za maisha; hapa ni eneo ambalo lina misigano mikali ya kidini na kisiasa; mambo yanayoleta changamoto kubwa katika mchakato wa upatanisho, haki, amani na utulivu.

Askofu mkuu Dal Toso anasema, katika machafuko na kinzani za namna hii katika Ukanda wa Sahel, ushuhuda na mshikamano wa upendo na mambo msingi sana yanayopewa kipaumbele cha kwanza na Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Ni mwaliko wa kuendeleza majadiliano ya kidini, kwa kutambua kwamba, Kanisa linapenda kuwa ni chombo cha haki, amani na upatanisho kati ya Watu wa Mataifa; ili kwa pamoja waweze kujifunga kibwebwe kupambana na Jangwa ambalo linazidi kutishia ustawi na maendeleo ya wananchi wa Ukanda wa Sahel. Hili ndilo lengo kuu lililomsukuma Mtakatifu Yohane Paulo II kuamua kuanzisha Mfuko wa Sahel, ili kusaidia kukoleza mchakato wa maendeleo ya watu katika Ukanda huu kunako mwaka 1980.

Papa Yohane Paulo II aliwataka wajumbe wa Mfuko huu kuhakikisha kwamba, wanajielekeza zaidi katika mafunzo makini kwa wadau ambao watasimama kidete kupambana vyema na uharibifu wa mazingira, hali ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa kuenea kwa Jangwa la Sahel. Ukame wa kutisha katika Ukanda wa Sahel ni matokeo pia ya mabadiliko ya tabianchi, hali ambayo imesababisha maafa makubwa kwa watu na mifugo yao.

Ukame wa kutisha umechangia pia ongezeko kubwa la watoto wenye utapiamlo wa kutisha pamoja na magonjwa ya milipuko. Tangu kuanzishwa kwake, Mfuko huu umepata mafanikio makubwa ambayo hayana budi kuendelezwa na wadau mbali mbali, ili kudhibiti kuenea kwa Jangwa la Sahel, lililosababisha maafa makubwa kati ya mwaka 1973 na mwaka 1974.

Mwenyeheri Paulo VI, Mtakatifu Yohane Paulo II, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na kwa sasa Papa Francisko ni viongozi wa Kanisa ambao wanajielekeza katika kuhamasisha utunzaji bora wa mazingira kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu pamoja na kupambana na baa la umaskini, njaa na maradhi, ndiyo maana Cor Unum, inaendelea kuwa bega kwa bega na wadau mbali mbali katika mchakato wa maboresho ya mazingira Ukanda wa Sahel.

Mafanikio ya miradi inayosimamiwa na kuendeshwa na Mfuko wa Yohane Paulo II kwa ajili ya sahel yanapimwa kwa kuangalia udhibiti wa Jangwa la Sahel na kwamba, kuna haja ya kujenga mahusiano mema na Makanisa mahalia kwani huu ni mchango wa Kanisa kwa ajili ya maendeleo ya Familia ya Mungu, Ukanda wa Sahel. Fedha ya Kanisa halina budi kutumiwa kwa malengo yaliyokusudiwa katika ukweli, uwazi na uwajibikaji sanjari na kupima matokeo ya mradi husika.

Wajumbe washirikishe tafiti, mafanikio na changamoto wanazokabiliana nazo katika mapambano ya kudhibiti kuenea kwa Jangwa, Ukanda wa Sahel, ili kukoleza maendeleo na kulinda mazingira.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.