2015-02-18 08:26:50

Haki!


Zingatieni haki na kutenda mema ndiyo kauli mbiu inayoongoza Ujumbe wa Kwaresima kwa Mwaka 2015 kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Maaskofu wanakazia haki; wanapembua ukuu wa haki na tunu zake; matendo mema kama ushuhuda wa imani. Maaskofu wanaangalia matukio ya Kikanisa hasa kuhusu maadhimisho ya Sinodi ya Familia na Mwaka wa Watawa Duniani. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linapembua kwa kina na mapana wajibu wa kijamii wa Kanisa kwa kuangalia kuhusu mchakato wa Katiba mpya na uchaguzi mkuu wa Mwaka 2015. RealAudioMP3

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, leo inakushirikisha utangulizi na sura ya kwanza ya ujumbe wa Kwaresima kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

Wapendwa Taifa la Mungu,
“Neema na iwe kwenu, na amani zitokazo kwa Mungu, Baba yetu” (Kol 1:2).
Tunapoanza kipindi cha Kwaresima, kipindi cha toba na uongofu wa nafsi zetu, “tujiandae kuruhusu nafsi zetu zitajirishwe kwa neema ya Ufufuko”.1 Maisha yote ya imani yetu yanatuelekeza katika tumaini la ufufuko. Katika kipindicha Kwaresima, imani inaimarishwa, matumaini ya kweli yanafufuliwa, upendo ulioanza kuchakaa unasafishwa na Pasaka ya milele inaandaliwa.

Hiki ni kipindi ambacho Kanisa,kupitia Neno la Mungu na mazoezi ya kiroho, linatukumbusha na kutuelekeza kurudi na kulielekea lengo la juu kabisa la maisha yetu katika uhusiano mkamilifu na Mungu. Ukamilifu wa uhusiano na Mungu, ambao kwao uhusiano wote wa binadamu unaratibiwa, unajengwa juu ya msingi wa wemana haki. Ndio maana, katika maadhimisho ya Kwaresima ya mwaka huu, sisi Maaskofu wenu, tunapenda kuungana nanabii Isaya tukiwahimiza na kusema: “Zingatieni haki na kutenda mema” (Isa 56:1).

Kama jamii ya waamini, tumesimama mbele ya wajibu wa maisha ambao unadai ukomavu na ujasiri wa kiimani. Wajibu huu ni wa kutenda haki kwa nafsi zetu wenyewe, yaani;kuutafuta wokovu wetu, na kuwa wema kwa kuwatendea jirani zetu wote haki kila tunaposaidiana na kuelekezana katika mambo yote yampendezayo Mungu na kuijenga jamii.

Tafakari hii ya Kwaresima tunaileta kwenu ili pamoja tuzipime njia na mienendo yetu ili kuona ni kwa kiasi gani tunazingatia haki na kutenda mema mbele ya Mungu na mbele ya jamii. Ni kwa njia hiyo tu ndipo tunapoweza kutambua ni kwa kiasi gani tumefanikiwa “kuidhihirisha harufu ya kumjua yeye kila mahali kwa kazi yetu!” (2Kor 2:14). Kama bado hatujaanzakuzingatia misingi ya haki na wema, hii ni fursa ya kuanza mara moja. Na Mungu atatuimarisha na kutuokoa kwani yeyemwenyewe anatamka: “Ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jinalangu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, nakuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia kutoka mbinguni, nakuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao” (2Nya 7:14).

SURA YA KWANZA

HAKI
Zingatieni haki na kutenda mema ninyi ambao mlioitwa na Mungu na kukombolewa na Bwana Wetu Yesu Kristo mpate kufanywa wenye haki na kustahili kupokea memayote ambayo Mungu amewaandalia watu wake. Ujumbehuu ulikuwa ni onyo kwa viongozi wa Waisraeli wa kizazi kilichofuatia kile kilichotoka utumwani Babeli, kizazi kilichokuwa na matumaini makubwa ya kuishi maisha huru na ya mafanikio ambayo kwa bahati mbaya hawakuyapata kutokana na umaskini uliokithiri, manyanyaso na kusetwa mikononi mwa wachache.

Maneno haya ambayo Mwenyezi Mungu anayatamka kupitia kinywa cha nabii Isaya ndio mwaliko ambao sisi Maaskofu wenu tunautoa kwenu Wanafamilia ya Mungu ili kila mwamini ajichunguze na kupima mwenendowake katika kuzingatia haki na kutenda mema. Msingi wa maisha yetu ni kumuonea Mungu kiu na kuishi katika njaa isiyokoma ya kutenda mema kwa ajili ya Mungu.

Mungu ni haki. Na kila inapotokea mwanadamu akatenda mema anakuwa ametenda haki. Haki ni “utashi wa kudumu wa kumpa Mungu na jirani iliyo haki yao”.2 Mungu na jirani ni sehemu ya lazima katika safari ya maisha yetu. Kuumbwa kwetu kwa sura na mfano waMungu (Mwa 1:26) kumetuweka chini ya wajibu wa kuwakielelezo cha haki na wema wa Mungu katika maisha yetu. Tunapoutimiza wajibu huu adhimu Mungu anaishibisha njaa yetu na kuponya kiu yetu (Mt 5:6). Kwa upendomkubwa Mungu aliiumba dunia na vyote vilivyomo nakwa haki yake anatawala dunia na kuiongoza.

Ni kwa wema na upendo mkubwa alimwumba mwanadamu na kumpa hadhi na heshima kubwa kati ya viumbe vyake vyote. Hata pale mwanadamu alipomkosea muumbawake, Mungu alimwadhibu kwa haki na kwa wema wake akaanzisha mpango mkubwa wa ukombozi. Mwenyezi Mungu aliendelea kuonesha upendo, wema na haki yake kwa taifa teule kipindi chote cha mahangaiko utumwani Misri na baadaye jangwani alipowaongoza wana waIsraeli kwa miaka 40.

Ni kwa wema, upendo na haki yake aliwainua waamuzi na baadaye manabii wapate kuwaelekeza watu wakena kwa mkono wa watawala aliwateua, aliwaongoza nakuwafanya taifa kubwa ingawa mara nyingi walimwachana kumwasi. Utimilifu wa upendo na wema wa Mungukwa wanadamu unaonekana katika nafsi ya Bwana wetu Yesu Kristo aliyesulubiwa ili wanadamu wapate kuhesabiwa haki: “Kwa maana jinsi hii Mungualiupenda Ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee bali awe na uzima wa milele!” (Yn 3:16).

Kumjua Mungu ni kutenda haki (Yer 22:16). Ni katika huruma kuu na wema wake Mungu, Neno alifanyika mwili na kukaa kwetu nasi tukauona utukufu wake, amejaa neema na kweli. Katika maisha na utume wake Bwana Wetu Yesu Kristo alipita huko na huko akitangaza habari njema kwa maneno na matendo yake. Kwa hotuba ya mlimani anatoa ufupisho wa mafundisho yake; “heri walio maskini wa roho, maana ufalme wa mbinguni ni wao” (Mt 5:3-11) na kwa maneno ya nabii Isaya anadhihirisha na kutoa dira ya utume wake; “roho ya Bwana i juu yangu, kwa sababu Bwana amenitia mafuta,niwahubiri wanyenyekevu Habari Njema. Amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao” (Is 61:1). Kwa wema mkubwa anaponya wagonjwa, anafufua wafu, analisha wenye njaa na kwa huruma kuu anasamehe wenye dhambi. Ni katika mwanga wa haki ya kimungu Kristo anatetea wanyonge na kuwashutumumafarisayo na walimu wa sheria.

Kanisa lililo chombo cha wokovu wa wanadamu linabidishwa kupokea mwaliko wa kuzingatia haki nakutenda mema kama msingi wa utume wake kwa karne zote. Kanisa linao wajibu wa msingi kabisa wa kulindana kutetea haki na kujibidisha kwa huruma na ukarimu kuwatetea watu wote hasa wanyonge na waliosahaulika. Pamoja na jukumu hili, Kanisa linatambua kuwa linapaswa kuongozwa na kutekeleza utume wake kwa haki, upendo na ukarimu kwa wote.

Ni katika mwanga huu jamii ya waamini katika ujumla wake na hatamwamini mmoja mmoja anaalikwa kuzingatia haki na kutenda mema kwanza kabla ya kutafuta haki na kudai kutendewa mema kama anavyofundisha Mt. Fransisko wa Asizi katika sala yake: “Ee Bwana unifanye chombo cha amani yako, nieneze mapendo palipo na chuki, walipokoseana nilete msamaha, nilete mwanga palipo na giza, nilete furaha palipo na huzuni… Ee Bwana unijalienitamani zaidi kufariji kuliko kufarijiwa, kufahamukuliko kufahamiwa, kupenda kuliko kupendwa”.

Jiunge nasi tena katika mwendelezo wa tafakari ya Ujumbe wa Kwaresima kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.