Kardinali Berhaneyesus Derew Souraphiel, ni kati ya Makardinali wapya 20 waliosimikwa
rasmi na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 14 Februari 2015 katika Ibada
iliyofanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Kutoka Barani Afrika,
Kanisa limewapata Makardinali wapya watatu, jambo la kumshukuru Mungu. Kardinali Souraphiel
anasema, Kanisa bado linawajibu wa kuwa ni sauti ya wanyonge, maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa jamii, kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima
yao kama binadamu. Kanisa ni sauti ya kinabii kwa wale wasiokuwa na sauti, ni mtetezi
wa wanyonge, kwani Kanisa ni sauti ya kimaadili. Sauti ya Familia ya Mungu Barani
Afrika inapaswa kusikika, kwani kuna watu wanaoteseka na kunyanyasika kutokana na
umaskini, ujinga na maradhi wakati ambapo kuna raslimali nyingi ambazo zingeweza kuiendeleza
Familia ya Mungu Barani Afrika. Kardinali Souraphiel anapongeza changamoto zinazoendelea
kutolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa hususan katika
mabadiliko ya Sekretarieti kuu ya Vatican, mada ambayo imejadiliwa na Makardinali
katika mkutano wao wa siku mbili hapa mjini Vatican. Anasema, Baba Mtakatifu anapenda
kukazia dhana ya Kanisa la Kiulimwengu, kwa kuwa na wawakilishi kutoka sehemu mbali
mbali za dunia, ili kujenga Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume. Makardinali
wapya 20 kutoka katika nchi 18 wanaonesha mwelekeo wa mabadiliko makubwa yanayoendelea
kufanywa na Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa. Ikumbukwe
kwamba, Makardinali ndio washauri wakuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika utekelezaji
wa dhamana na utume wake kwa Kanisa la Kristo na kwamba, hiki si cheo cha heshima.
Makardinali wataendelea kumsaidia Baba Mtakatifu kwa kuchangia kadiri ya uwezo wao,
ustawi na maendeleo ya Kanisa. Hapa Kanisa halina budi kujipambanua anasema Kardinali
Souraphiel kwa kuwa ni sauti ya wanyonge na maskini, kwa kusimama kidete kulinda,
kutetea utu na heshima ya binadamu, ustawi na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko
anataka kuliona Kanisa maskini kwa ajili ya huduma kwa maskini; Kanisa ambalo daima
linafanya hija ya maisha na watu wakati wa raha na shida, wakati furaha na shangwe.
Hapa mtu na utu wake wanapewa kipaumbele cha kwanza kuliko mambo mengine yote. Anakazia
mshikamano wa upendo na udugu; majadiliano ya kidini na kiekumene. Ni kiongozi anayependa
kuwatetea wanyonge na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Papa Francisko amekuwa
ni msemaji mkuu na mtetezi wa wahamiaji kutoka Barani Afrika wanaoendelea kufariki
dunia huko kwenye Bahari ya Mediterrania, wakiwa na matumaini ya kufika Ulaya, ili
waweze kuboresha maisha yao, lakini ndoto zote hizi zinapotelea katika tumbo la Bahari
ya Mediterrania kama yalivyo machozi ya samaki yanaishia majini. Kuna haja ya kupambana
kufa na kupona na wafanyabiashara haramu wa binadamu, ili kukomesha utumwa ambao unaendelea
kudhalilisha utu na heshima ya binadamu. Bara la Afrika halina budi kuwekeza katika
elimu, ili kuwakomboa wananchi wengi kutoka katika lindi la ujinga na maradhi. Kuwepo
na mikakati na sera nzuri zitakazozalisha ajira kwa vijana, ili waweze kuondokana
na ndoto ya mchana kwamba, maisha mazuri yanapatika Ulaya! Elimu inaweza kuwasaidia
vijana kuboresha maisha yao hatua kwa hatua. Ni matumaini ya Kardinali Souraphiel
kwamba, iko siku, Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, ataweza kutembelea
Ethiopia na hatimaye, kupata nafasi ya kuzungumza na viongozi wa Umoja wa Afrika.
Baba Mtakatifu anaendelea kukazia kwamba, uongozi ni huduma na wala si ujiko! Na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, kwa msaada
wa NCR.