Kabla ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Mama Kanisa ametuwekea utaratibu
wa kuchunguza dhamiri zetu, ili kuomba toba na msamaha wa dhambi na hatimaye kuadhimisha
mafumbo ya Kanisa kwa ibada na uchaji mkuu. Ebu chukua muda kidogo ufanye tafakari
kuhusu sala hii katika maisha yako ya kila siku! "Namuungamia Mungu Mwenyezi, nanyi
ndugu zangu kwani nimekosa mno; kwa mawazo, kwa maneno, kwa matendo na kwa kutokutimiza
wajibu. Nimekosa mimi, nimekosa mimi, nimekosa mno. Ndiyo maana namwomba Bikira Maria
mwenye heri, Mama wa Mungu, Malaika na Watakatifu wote, NANYI NDUGU ZANGU niombeeni
kwa Bwana Mungu wetu" Sala hii huwa tunaisali karibu kila siku, na kila tushirikipo
Ibada ya Misa Takatifu. Ni sala ambayo tumeizoea sana katika maisha yetu ya kila siku.
Leo kwa namna ya pekee tuirudie sala hii na kisha tutafakari baadhi ya vipengele vyake
hasa nafasi ya ndugu katika maisha yetu ya kawaida ya kila siku na yale ya utakatifu.
Ndugu zetu, hasa, wazazi wetu, wenza wetu wa ndoa, wanafamilia, ndugu wa mbali
na wa karibu, jamaa zetu, marafiki, wafanyakazi wenzetu n.k Je, wana nafasi gani katika
maisha yetu? Tunaitambua nafasi yao muhimu katika maisha yetu? Tunawatendea haki na
kuiheshimu nafasi yao?
Mara nyingi hatufahamu nafasi yao na hivyo huwa tunawakosea
sana; tunawatukana, tunawakasirisha, tunawasengenya, tunawahukumu, tunawashudia uongo,
tuwadhulumu, tunawatapeli, tunawaomba rushwa, tunawazulia mabaya na kuwaombea yawapate
mabaya, tunawaharibia, kuwaficha na kuwazibia fursa zao za maendeleo. Hatutumizi wajibu
zetu kwao kama wazazi, wakubwa, wazee wa jamii, kama watoto, viongozi na kuliko yote
kama wakristu. Wajibu hizi ni pamoja na kuwashauri, kuwakosoa, kuwakemea, kuwapa
mahitaji ya kila siku, kuwaongoza vyema ili kitimiza wajibu zao na kutenda mema, kuwapenda. Hao
ndugu zetu wana nafasi kubwa sana katika maisha yetu km nilivyosema hapo juu. Wana
nafasi ya kuturekebisha, kutuombea, kutusaidia ktk mambo mbalimbali, wa kutuonesha
na kuuona ukuu wa Mungu kwao. Hao ndiyo tunaoishi nao kila siku, wanatufahamu vizuri
sana. Vitabu vinatuambia kuwa hatuwezi kusema kuwa tunampenda Mungu ambaye hatumuoni
wakti tunamchukia mwanadamu mwenzetu tunayeishi naye kila siku. Kwa kumpenda na kumjali
mwanadamu mwenzetu tutakuwa tunampenda Mungu na lolote tunalomtendea mwanadamu mwenzetu
tunamtendea Mungu. Wapendwa, tunaingia katika kipindi cha Kwaresma, kipindi cha
toba, ni wakati wa kutafakari utajiri na tunu iliyofichika katika ndugu zetu, tujichunguze
na kuona kwa kiasi gani tulikosa, tumekosa na tunaendelea kukosa kwao. Sala hii itutafakarishe
nafasi ya ndugu zetu katika ukombozi wetu. Ni kipindi cha kutubu, kuombana msamaha
na kusameheana. Tukitumie kipindi hiki cha Kwaresma tunachokianza kwa kupakwa majivu,
alama ya toba ili kurudisha mahusiano mema katika familia zetu, makazini, kwenye Jumuiya,
makanisani na katika jamii kwa ujumla. Tuache kiburi na kisirani na kujiona sisi ni
watenda haki zaidi kuliko wenzetu, tuwe wepesi wa kutenga muda wa kutafakari maisha
yetu na nafasi ya ndugu zetu katika maendeleo na katika wokovu wetu. Tushiriki
kiaminifu matukio mbalimbali katika kipindi hiki. Hayo ni pamoja na Jumatano ya Majivu
ambayo ni siku ya kufunga chakula, njia ya msalaba kila Ijumaa, tafakari za mateso,
semina za kukua kiroho, matendo ya huruma kwa kuwajali ndugu zetu wahitaji na kuwapelekea
kile tulichojinyima katika kipindi hiki. Tuhitimishe na Juma kuu la mateso. Tujiepushe
na matendo maovu na starehe za kidunia. Mwisho wa kipindi hicho cha Kwaresma, tujifanyie
tathmini kama tumebadilika kiasi gani. Nawatakieni wote mwanzo mwema wa kipindi cha
Mfungo na Toba. Tumsifu Yesu Kristo ! Na Antipasi Shinyambala Jimbo kuu
la Dar es Salaam.