2015-02-17 09:46:07

Ngumi bungeni!


Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini limesikitishwa sana na uvunjifu wa misingi ya haki, amani na demokrasia nchini humo wakati Chama cha Upinzani, kilipoamua kumzomea na kumfanyia vurugu Rais Jacob Zuma wakati alipokuwa analihutubia Bunge la Afrika ya Kusini hivi karibuni.

Polisi ililazimika kuwatoa nje wabunge wa vyama vya upinzani waliokuwa wanamshutumu Rais Zuma kwa rushwa na ufisadi wa mali ya umma. Wabunge wa upinzani wanataka kufahamu kwa nini Rais Zuma alitumia fedha ya walipa kodi kwa ajili ya kufanya ukarabati mkubwa kwenye jumba lake la fahari huko Nkandla.

Baraza la Maaskofu Katoliki linalaani vikali ukosefu wa nidhamu na maadili uliooneshwa na wabunge kutoka chama cha upinzani na kwa upande mwingine wanalishutumu Jeshi la Polisi kwa kutumia nguvu kupita kiasi na hivyo kuvuruga haki ya Bunge. Maaskofu wanasema wananchi wana haki ya kufahamu kile kinachotendeka Bungeni na harakati za kutaka kuficha ukweli ni kwenda kinyume cha Katiba ya Nchi inayotoa uhuru kwa wananchi kufuatilia kwa umakini mkubwa masuala ya vikao vya Bunge.

Baraza la Maaskofu Katoliki, mwishoni mwa tamko lao wanamsihi Rais Jacob Zuma kutoa ufafanuzi wa kina kwa Bunge na kwa Taifa kuhusu matumizi mabaya ya fedha ya umma. Vitendo vya kihuni vilivyofanywa na baadhi ya wabunge wa upinzani vimechafua mchakato wa demokrasia na kwamba, wananchi wa Afrika ya Kusini wanahitaji kuona demokrasia pana zaidi.

Itakumbukwa kwamba, Rais Jacob Zuma alichaguliwa kwa awamu ya pili kunako mwaka 2014 licha ya kuandamwa na kashfa ya ufisadi na ubadhilifu wa mali ya umma. Lakini, Serikali imetetea uamuzi wa Rais Zuma kufanya ukarabati mkubwa katika Jengo lake kwani ni kwa ajili ya usalama.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.