Chuo kikuu cha Kipapa cha Gregorian kilichoko mjini Roma, Jumatatu tarehe 16 Februari
2015 kimezindua Kituo maalum kwa ajili ya kulinda watoto. Baba Mtakatifu Francisko
katika tukio hili, amemtumia ujumbe wa matashi mema, Padre Hans Zollner pamoja na
wafanyakazi wote wanaojisadaka kwa jili ya ulinzi, malezi na makuzi bora ya watoto
dhidi y anyanyaso za kijinsia.
Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza
wote kutoka katika undani wa moyo wake. Ni matumaini yake kwamba, kazi hii njema itaweza
kuzaa matunda yanayokusudiwa kwa wakati wake. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea
kuwaombea na kuwaweka chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria na anawaomba wao
pia kumsindikiza kwa njia ya sala katika maisha na utume wake.
Itakumbukwa
kwamba, hivi karibuni, Tume ya Kipapa ya ulinzi kwa watoto imehitimisha mkutano wake
wa kwanza kwa kukazia umuhimu kwa viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba, wanaunda
mazingira bora na salama kwa makuzi ya watoto. Kutokana na unyeti wa suala lenyewe,
wajibu huu unapaswa kutekelezwa kwa makini kwa kuzingatia sheria, kanuni na misingi
bora ya maadili.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili
ya Radio Vatican.