Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuhakikisha kwamba, mchakato wa maendeleo na maboresho
katika sekta ya uchumi unakwenda sanjari na kanuni msingi za maadili na utu wema,
mwanadamu akipewa kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya kiuchumi, vinginevyo,
mkwamo wa uchumi utaendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu sehemu mbali mbali
za dunia. Ni changamoto ambayo imetolewa hivi karibuni na Kardinali Oscar Andrès
Rodrigues Maradiaga, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki
Kimataifa, Caritas Internationalis, wakati wa kuzindua kitabu kilichoandikwa na Bwana
Andrea Tornielli kuhusu mchakato wa ukuaji wa uchumi kadiri ya mafundisho ya Baba
Mtakatifu Francisko. Kuna haja ya kuwa na ujasiri wa kubadili sera na mfumo wa
uchumi ikiwa kama hautowi kipaumbele cha kwanza kwa binadamu, utu na heshima yake.
Tabia ya kujinyima kwa ajili ya mafao ya maisha ya kiroho na kimwili ni fadhila ya
Kikristo, lakini kuwalazimisha watu kufunga mikanda kiasi cha kuwatesa baadhi ya wananchi
kwa kuwasukumiza pembezoni mwa jamii, wakati wengine wakiendelea kula kuku kwa mrija
si jambo la haki na wala halipendezi machoni pa Mungu. Sera za uchumi wa namna hii
ni mauaji kwa watu wasiokuwa na hatia. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka
wake wa kichungaji Injili ya Furaha anafafanua kwa kina na mapana umuhimu wa sera
na mikakati makini ya kiuchumi inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu, utu na
heshima yake. Mkazo ni kuhakikisha kwamba, wananchi wanapata huduma msingi katika
sekta ya elimu, afya na maendeleo. Wananchi wapate fursa za ajira ili kuzitegemeza
familia zao, sanjari na kuendeleza mchakato wa upendo na mshikamano kati ya watu unaoongozwa
na kanuni auni; mambo msingi kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa; ambayo wataalam
wengi wa uchumi wanayasahau, lakini ni muhimu sana kwa ustawi na maendeleo ya binadamu
wote, kwani hapa kipaumbele cha kwanza ni binadamu na mafao ya wengi. Bwana Andrea
Tornielli mwandishi wa kitabu hiki anasema, lengo ni kuwachangamotisha wataalam na
watunga sera za uchumi na maendeleo kufungua macho, ili kuona pia mchango wa Mafundisho
Jamii ya Kanisa katika ustawi na maendeleo ya binadamu badala ya kuendelea kujikita
katika sera za uchumi ambazo zimejielekeza zaidi katika taasisi za fedha ili kutafuta
faida kubwa na matokeo yake ni athari za myumbo wa uchumi kimataifa, jambo ambalo
kwa sasa ni janga la watu wengi, kwani ukuaji wa uchumi unaendelea kusua sua licha
ya sera na mikakati iliyobainishwa na kupangwa na wachumi waliobobea katika fani hii. Mshikamano
wa upendo ni dhana ambayo pia haina budi kumwilishwa katika uhalisia wa sera na mikakati
ya maendeleo endelevu, kwani hili ni jambo linalowezekana kabisa na wala hapa si kutetea
wala kulinda siasa ya kikomunisti, kama ambavyo Baba Mtakatifu Francisko anavyobainisha
katika mahojiano maalum na mwandishi wa kitabu hiki, kwani upendo na mshikamano ni
tunu ambazo hazina mipaka wala vizingiti. Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.