2015-02-16 09:26:51

Watakatifu wapya kutangazwa hapo tarehe 17 Mei 2015


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 14 Februari 2015 baada ya kuwasimika rasmi Makardinali walioteuliwa hivi karibuni katika Ibada ya Liturujia ya Neno la Mungu iliyofanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican; Makardinali katika sehemu ya pili, walipitisha majina ya watakatifu wanne watakaotangazwa na kuandikwa kwenye orodha ya majina ya watakatifu wa Kanisa hapo tarehe 17 Mei 2015.

Watakatifu wapya watakaotangazwa ni: Yohana Emilia de Villeneuve, Maria wa Yesu Msulubiwa Baouardy, Maria Alphonsina Ghattasare pamoja na Maria Cristina wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili ambaye tayari Makardinali walikwisha ridhia kwamba, aandikwe kwenye orodha ya Watakatifu katika mkutano wa Makardinali uliofanyika tarehe 20 Oktoba 2014.

Watakatifu wote wanne wanaotarajiwa kutangazwa wote ni watawa: wawili ni kutoka katika Nchi Takatifu, Italia na Ufaransa. Tukio hili litafanyika wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka wa Watawa, ili kuwaamsha walimwengu kwa njia ya ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.