2015-02-16 10:44:00

Dumisheni mahusiano mema!


Mpendwa msikilizaji wa Kipindi chetu cha Kanisa la Nyumbani, tumsifu Yesu Kristo, Laudetur Iesus Christus! Kwa mara nyingine tena tuendele kuzichambua hati za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ambamo Mama Kanisa anatufundisha mambo mbalimbali yenye kutujenga katika Ukristo wetu. RealAudioMP3

Katika vipindi vilivyopita, baada ya kuyatupia macho matamko yale mawili yaani Gravissimum educationis (tamko lililohusu uzito wa malezi) na Dignitatis humanae (tamko lililohusu uhuru wa dini), leo mpendwa msikilizaji tulitegee sikio tamko la tatu linalohusu uhusiano wa Kanisa na dini zisizo za Kikristo, kwa lugha ya Kilatini tamko hili linaitwa Nostra Aetate, likimaanisha Wakati Wetu!

Mtaguso Mkuu ulizingatia ukweli kwamba watu wa wakati wetu wanazidi kuunganishwa kwa namna mbalimbali, na kunaonekana utegemeano dhahiri kati ya watu wa mataifa mbalimbali ya dunia. Ni kwa ukweli huo, Kanisa nalo linahimiza tabia ya mahusiano mema na dini zisizo za Kikristo. Linahamasisha umoja na upendo kati ya wanadamu, kati ya mataifa mbalimbali kwa sababu watu wote ni jumuiya mmoja, asili yao ni mmoja, na ni Mungu ndiye aliyewaweka wote wakae juu ya uso wa nchi.

Ndani ya Nostra aetate, yaani Wakati Wetu, Kanisa linazitazama dini mbalimbali kama ishara ya kiu ya mwanadamu ya kutaka kujua ukweli wa ndani juu ya uumbaji, maisha, mateso, kifo na maisha baada ya kufa. Katika dini zote, mwanadamu anakiri uwezo fulani mkuu ambao ni chanzo na kikomo cha yote. Daima mwanadamu huyu hutafuta muungano na hiyo Nguvu kuu, ambayo kwayo husaidiwa kupata maana ya uhalisia wa maisha ya kila siku. Pamoja na mambo mengine mengi, katika dini mwanadamu ataka kujua binadamu ni nini, maana na mwisho wa maisha yake ni nini, dhambi na tendo jema ni nini, chanzo na lengo la mateso ni nini, njia gani inatupeleka kwenye furaha ya kweli, mauti na hukumu ni nini. Zaidi pia binadamu ataka kujua, anatoka wapi na anakwenda wapi.

Nostra aetate, Wakati Wetu, yatuambia; Kanisa Katoliki linaamini ukweli wa Kihistoria kwamba, tangu zamani za mwanadamu dini mbalimbali zimekuwa ni kielelezo cha hiyo kiu ya mwanadamu, na hivyo linaheshimu sana mambo yote yaliyo kweli na matakatifu katika dini nyinginezo. Linaheshimu kwa sifa timamu sheria zote na mafundisho ambayo yana mwanga fulani wa ukweli wa kuwaangazia watu, hata kama mambo hayo ni kinyume cha yale ambayo Kanisa lenyewe linasadiki na kufundisha. Pamoja na kuheshimu ukweli huo ulioko katika dini nyinginezo, Kanisa na waana Kanisa ni lazima kuendelea kumsadiki na kumtangaza Kristo Yesu aliye njia, ukweli na uzima.

Ndani ya Nostra aetate, Kanisa latuhimiza kutoa ushuhuda wa imani ya Kikristo kwa busara na mapendo, kwa njia ya majadiliano na ushirikiano na wafuasi wa dini nyinginezo, na zaidi ya hayo, Mama Kanisa anatuambia sisi Wakristo, tujibidishe kutambua na kukuza mema ya kiroho na ya kimaadili na tunu za kijamii na za kitamaduni zinazopatikana kwa ndugu zetu wasio wa-Kristo.

Mpendwa Msikilizaji, kwa njia ya Nostra aetate, Kanisa linatuhimiza sisi sote kuishi kwa amani, umoja, upendo na ushirikiano, kama jumuiya mmoja inayounganishwa kwa pendo la Mungu Baba. Kwa nini leo watu wanaleta mafarakano duniani kwa jina la dini? Mama Kanisa daima anafundisha na kutuhimiza ‘tutambuane katika tunu zilizomo kwa kila mmoja wetu, na tuheshimiane katika tofauti zetu. Sote ni watoto wa Baba mmoja, ambaye ni Mungu, na sote tunajibidisha kumpenda, kumtumikia na kumwendea yeye kwa njia mbalimbali. Kwa nini tudharauliane?
Mpendwa msikilizaji wa Kanisa la nyumbani, neno hili linakujia sikioni pako kabisa; ‘wewe na mimi, tujitahidi kuwaheshimu wengine katika dini zao. Pili, tujibidishe kuwaelewa wale ambao hawaamini kili tunachokiamini sisi, ili tuone tunu za mwanga wa ukweli zinazowaongoza kwa Mungu. Tatu tutawale sana utashi wetu na midomo yetu, ili wewe au mimi mmoja wetu asiwe msemaji wa dini ya mwenzake. Kila mtu aisemee na kuifafanua dini yake mwenyewe. Ukishika kipaza sauti na kumfungia mwenzako spika-mzinga dirishani ili kuikashifu dini yake, hapo utasambaratisha upendo na amani itawekwa rehani.
Daima ikumbukwe, nafsi ya mtu imeunganika kwa fumbo la ajabu sana na ukweli kuhusu dini. Pale unapoikejeli dini ya mtu, ni kama unakejeli nafsi yake na mtaala mzima wa maisha yake. Mtu aheshimiwe tu katika imani yake. Iwapo kuna jambo unahitaji kuelewa katika dini fulani, basi waulize kwa upole wahusika, wakufafanulie. Na ukishafafanuliwa na ukaona tunu zao hazikusadifu, usiwakashifu wala kuwadharau, nyamaza kimya uwaheshimu. Ni kwa upole na heshima, tutajenga upendo.
Kwako mpendwa Mkatoli, sauti pole ya Mama Kanisa inatuagiza, kamwe tusiwe chanzo cha chokochoko za kidini. Imani, matumaini, mapendo, amani, utulivu, heshima na maelewano mema, daima viwe dira yetu.
Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB








All the contents on this site are copyrighted ©.