2015-02-15 08:36:59

Tuzo ya Kimataifa kwa Radio Vatican!


Maadhimisho ya Siku ya Radio Kimataifa yaliyofanyika hivi karibuni, ilikuwa ni fursa pia kwa Radio Vatican kufanya kumbu kumbu ya miaka 84 tangu ilipoanzishwa. Kwa namna ya pekee maadhimisho haya kwa Mwaka 2015 yameacha chapa ya kimataifa kwa Radio Vatican kutunukiwa Tuzo ya Radio Kimataifa kutoka Hispania, iliyopokelewa na Askofu mkuu Renzo Fratini kwa niaba ya Radio Vatican.

Padre Federico Lombardi, Mkurugenzi mkuu wa Radio Vatican katika ujumbe wake kwa njia ya video katika tukio hili anabainisha kwamba, Radio Vatican inaendeleza dhamana na historia yake kwa kujipambanua zaidi kuwa ni Radio kwa ajili ya huduma ya Kanisa, ili kusaidia mchakato wa majadiliano, umoja na mshikamano wa Watu wa Mungu. Ni Radio ambayo inatoa huduma kwa Baba Mtakatifu na Kanisa katika ujumla wake na kwamba, itaendelea kusoma alama za nyakati kwa kukabiliana na changamoto za maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari, ili kuweza kuwafikia Watu wa Mataifa kwa urahisi zaidi.

Radio Vatican inajipambanua kwa kujikita zaidi na zaidi katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki na amani kwa kutambua kwamba, hivi ni vikolezo vya maendeleo endelevu ya binadamu. Radio Vatican inachochea majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga na kuimarisha upendo na mshikamano kati ya Familia ya Mungu, binadamu akipewa kipaumbele cha kwanza. Ni Radio ambayo imejitahidi kuwa ni sauti ya wanyonge na wale wasiokuwa na sauti; watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, changamoto na himizo la kuendelea kufuata sera na mikakati ya shughuli za kichungaji zinazotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, kwa kuwaendea watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii: kiroho na kimwili.

Padre Lombardi anasema, Radio Vatican inarusha matangazo yake katika lugha 40 za kimataifa na kati ya lugha hizi, kuna Lugha ya Kiswahili, kwa taarifa yako na kwamba, imeajiri wafanyakazi kutoka katika mataifa 60, bila kusahau kwamba, kuna wafanyakazi pia wanaotoka Afrika Mashariki. Kikosi kazi hiki kinaonesha ile ari na nguvu ya amani na majadiliano kwa watu wa nyakati hizi, ili kuweza kukabiliana na changamoto, matatizo na fursa mbali mbali zinazojitokeza katika maisha ya mwanadamu.

Padre Lombardi ambaye ni gwiji katika tasnia ya habari anasema kwamba, kiini cha huduma ya matangazo yanayotolewa na Radio Vatican katika medani za mawasiliano ya kijamii ni kuendeleza mchakato wa majadiliano, ili kukuza na kudumisha umoja wa Familia ya Mungu duniani. Huu ni utume unaofanyiwa kazi na Radio Vatican, kwa kuongozwa na ari pamoja na moyo wa Kiinjili kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko.

Padre Federico Lombardi anahitimisha ujumbe wake kwa kuwashukuru wadau waliouona mchango wa Radio Vatican katika ustawi na maendeleo ya binadamu, kiasi cha kuipatia tuzo hii ya kimataifa, jambo ambalo linatia nguvu na faraja ya kuendelea kushikamana na kushirikiana na wadau mbali mbali katika tasnia ya mawasiliano ya jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican







All the contents on this site are copyrighted ©.