Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, mara baada ya kuadhimisha
Ibada ya Misa Takatifu na Makardinali wapya, Jumapili tarehe15 Februari 2015, akiwa
kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican anasema kwamba, Mwinjili
Marko katika majuma kadhaa anamwosha Yesu anayewaokoa wagonjwa wa kiroho na kimwili;
Yesu anayepambana na Pepo wachafu, Yesu anayeshinda nguvu ya giza mahali popote pale
anapopita na kupewa nafasi!
Baba Mtakatifu Francisko anasema, wagonjwa wa Ukoma
walikuwa wanatengwa na jamii, lakini mgonjwa wa Ukoma baada ya kumwomba Yesu, anaponywa
kwa kuoneshwa na kuguswa na huruma pamoja na upendo wa Mungu, kielelezo kwamba, upendo
wa Mungu unavuka vizingiti vyote vya maisha. Yesu kwa njia ya ubinadamu wake, ameamua
kujitwika magonjwa na mahangaiko ya binadamu, ili aweze kuwakomboa, changamoto na
mwaliko kwa waamini kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya
Upatanisho.
Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Mwenyezi Mungu, kwa njia ya Yesu
Kristo anajitwalia hali ya ubinadamu, anateseka hadi kufa Msalabani, ili kumkomboa
mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na kwamba, Yesu anapambana na dhambi
kwa nguvu ya upendo na huruma ya Mungu. Ili waamini waweze kuwa kweli ni wafuasi amini
wa Yesu hawana budi kuungana kikamilifu na Yesu mwenyewe, ili kuwa ni vyombo vya upendo
na huruma yake, kwa wagonjwa, maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.
Waamini wanahamasishwa kujiachilia ili waguswe na kuambukizwa upendo wa Mungu.
Mwishoni
mwa Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu amewakumbuka watu kutoka Mashariki wanaojiandaa
kuadhimisha Mwaka Mpya, siku kuu inayowakirimia furaha, udugu na maisha ya kifamilia;
mambo muhimu katika maisha ya kijamii, changamoto ya kukuza na kuendeleza mahusiano
mema kati ya watu; kwa kujikita katika heshima, haki na upendo.
Kwa namna ya
pekee, Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea mahujaji wote waliofika mjini Vatican
ili kuungana na Makardinali wapya walipokuwa wanasimikwa rasmi, Jumamosi na katika
Ibada ya Misa Takatifu, Jumapili, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican.