Kardinali Berhaneyesus Demerew Souraphiel, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Addis Ababa
Ethiopia na Mwenyekiti wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki
na Kati, AMECEA anakuwa ni Kardinali wa pili kutoka nchini Ethiopia baada ya Kardinali
Paulos Tzadua, aliyefariki dunia kunako mwaka 2003.
Katika mahojiano maalum
na Radio Vatican anabainisha kwamba, changamoto kubwa iliyoko mbele ya Kanisa Barani
Afrika ni kuhakikisha kwamba linaendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene,
ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano kati ya watu.
Kanisa halina budi kujielekeza zaidi katika kuwaunganisha watu ambao kwa sasa wanasambaratika
kutokana na kinzani za kidini, kisiasa na kikabila, mambo ambayo yanakwamisha mchakato
wa maendeleo endelevu Barani Afrika na matokeo yake ni chuki, uhasama, rushwa na ufisadi
vinatawala miyo ya watu na kusahau mafao ya wengi.
Kardinali Souraphiel anasema
kwamba, Wakatoliki nchini Ethiopia ni wachache ikilinganishwa na Waamini wa Kanisa
la Kiorthodox, lakini ni waamini ambao wako imara na thabiti katika imani yao. Si
watu wanaoweza kuyumbishwa kwa urahisi, kwani wamefundwa wakafundika katika maisha
na utume wa Kanisa. Ni watu wanaotambua kwamba, imani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi
Mungu, inayopaswa kukumbatia, hadi kieleweke kama wanavyosema Waswahili. Waamini ambao
wana imani na matumaini kwa Kristo na Kanisa lake. Ni jamii inayoheshimu zawadi ya
Uhai na iko tayari daima kutangaza Injili ya Uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba
hadi mauti inapomfika mtu kadiri ya mpango wa Mungu
Kardinali Souraphiel anakiri
kwamba, kuna makundi makubwa ya vijana yanayohama kutoka Ethiopia kwenda kwenye Nchi
za Falme za Kiarabu ili kutafuta fursa za ajira na wengine wanathubutu hata kuhatarisha
maisha yao jangwani na baharini ili kutafuta maisha bora zaidi Barani Ulaya, lakini
kwa bahati mbaya, wengi wao wanakufa maji hata kabla ya kuona cheche za maisha bora
Barani Ulaya. Vijana wanaofaulu kufika Barani Ulaya, wengi wao wanajikuta wakitumbukizwa
katika biashara haramu ya binadamu, jambo linalodhalilisha utu na heshima yao.
Kardinali
Souraphiel anasema, Kanisa nchini Ethiopia linaendelea kuwahamasisha wanasiasa na
watu wote wenye mapenzi mema, kujikita katika mchakato wa maboresho ya maisha ya watu
wao, kwa kuwekeza katika huduma bora za elimu, afya na maendeleo ya jamii; kwa kutoa
kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu sanjari na mafao ya wengi. Hii
ni changamoto kubwa hata kwa Nchi za AMECEA ndiyo maana Kanisa nchini Ethiopia linaendelea
kuwekeza katika sekta ya elimu ambayo ni mkombozi wa wengi.
Kwa njia ya elimu
bora inayotolewa na Taasisi zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa, vijana wengi wataweza
kupata ujuzi na maarifa na hatimaye fursa za ajira. Kwa mtindo huu, vijana wanaweza
kuondokana na kishawishi cha kuikimbia nchi yao ili kwenda ughaibuni, ambako wanadhani
kuna "asali na maziwa", lakini huko siku hizi "kumejaa mbigili, ni patahiska nguo
kuchanika".
Elimu makini inawawezesha vijana kuwa na maadili mema na kuachana
na mambo ambayo yanaleta kichefu chefu na simanzi katika maisha ya kijamii. Ukosefu
wa fursa za ajira ni changamoto kubwa ambayo haina budi kufanyiwa kazi kwa umakini
mkubwa, kwani ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana kuna athari kubwa sana
katika kukoleza misingi ya haki, amani na utulivu. Vijana wasiokuwa na ajira mara
nyingi wamekuwa wanatumiwa na baadhi ya watu kusababisha kinzani na migawanyiko ya
kijamii, kwa kulipwa ujira kiduchu! Elimu inaweza kusaidia kupambana na majanga ya
kijamii, kwa kuimarisha maadili mema.
Kardinali Souraphiel anasema kwamba,
Familia Barani Afrika inapewa kipaumbele cha kwanza ndiyo maana Kanisa linaendelea
kujiwekea sera na mikakati ya kichungaji, ili kuzijengea familia za Kikristo uwezo
wa kutangaza kwa njia ya ushuhuda makini wa maisha Injili ya Familia, kwa kuendelea
kujikita katika tunu bora za maisha ya ndoa na familia. Kardinali Souraphiel anasema,
chezea kwingine, lakini Familia ni moto wa kutoea mbali.
Bado kuna shida na
changamoto nyingi zinazozikabili Familia nyingi Barani Afrika, kwa mfano umaskini
unaotokana na ukosefu wa fursa za ajira, unaowalazimisha akina baba kuacha familia
zao ili kwenda mbali kutafuta riziki ya maisha, kuna changamoto za malezi katika ndoa
mseto; kuna uwepo wa familia tenge inayosimamiwa na kuongozwa na mzazi mmoja; kuna
magonjwa ambayo yanawaacha watoto wengi wakiwa ni yatima pasi na msaada. Zote hizi
ni changamoto kubwa katika maisha na utume wa Familia Barani Afrika.
Ni matumaini
ya Familia ya Mungu Barani Afrika kwamba, Sinodi ya Maaskofu kuhusu Familia inayoongozwa
na kauli mbiu "Wito na utume wa familia ndani ya Kanisa na ulimwengu mamboleo" itaweza
kuibua sera na mikakati ya shughuli za kichungaji katika maisha ya ndoa na familia.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.