2015-02-14 14:56:16

Watakatifu watarajiwa!


Baada ya Baba Mtakatifu Francisko kuhitimisha Ibada ya kuwatangaza na kuwasimika Makardinali wapya 20, Ibada ya Liturujia ya Neno la Mungu iliingia sehemu ya pili kwa Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, amewasilisha Ombi la kuwatangaza Wenyeheri watatu kuwa Watakatifu kwa sifa na utukufu wa Mungu na Kanisa lake pamoja na kutangaza tarehe rasmi watakayoandikwa kwenye Orodha ya Watakatifu wa Kanisa.

Wenyeheri hawa ni:
1. Yohana Emilia wa Villeneuve.
2. Maria wa Yesu Msulubiwa Baouardy
3. Maria Alphonsina Danil Ghattasare.

Kardinali Amato baada ya kuonesha kwa Baba Mtakatifu kwamba, taratibu na mchakato mzima wa kuwatangaza Wenyeheri hawa kuwa Watakatifu umezingatiwa, aliendelea kusoma kwa ufupi, historia na wasifu wa watakatifu wapya watakaoandika katika Orodha ya Watakatifu kwa wakati muafaka.

Mwenyeheri Yohane Emilia wa Villeneuve alizaliwa nchini Ufaransa kunako mwaka 1811. Ni Mwanzilishi wa Shirika la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili kwa ajili ya elimu kwa watoto maskini, kwa ajili ya wagonjwa na shughuli za kimissionari. Alifariki dunia kwa ugonjwa wa Kipindupindu kunako tarehe 2 Oktoba 1854. Akatangazwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kuwa Mwenyeheri kunako mwaka 2009.

Mwenyeheri Maria wa Yesu Msulubiwa Baouardy alizaliwa Nazareth kunako mwaka 1846. Akabatizwa kwenywe Kanisa Katoliki la Wamelkiti. Tangu utotoni mwake, alikumbana na mahangaiko ya ndani, akabahatika kupata maono. Aliingia Shirika la Wakarmeli wa Pau, nchini Ufaransa. Ili kuwafunda Wakarmeli wapya alitumwa nchini India na baadaye akapelekwa Bethlehemu, alikofikwa na mauti kunako mwaka 1878. Alitangazwa kuwa Mwenyeheri na Baba Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1983.

Mwenyeheri Maria Alphonsina Danil Ghattasare, alizaliwa mjini Yerusalem kunako mwaka 1843. Akiwa na umri wa miaka kumi na mitano, alijiunga na Shirika la Watawa wa Mtakatifu Yosefu. Ni mtawa aliyejisadaka kwa ajili ya wasichana na wanawake Wakristo. Aakawa na Ibada ya pekee kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu. Ni mwanzilishi wa Shirika la Watawa wa Rozari takatifu Yerusalemu. Alifariki dunia kunako mwaka 1927 na kutangazwa kuwa Mwenyeheri na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kunako mwaka 2009.

Na padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.